Tafuta

👉 UMASKINI NA AFYA YA MSICHANA👇✔

UMASKINI NA AFYA YA MSICHANA.

Wasichana wengi wanaoishi katika nchi zinazoendelea hukabiliwa na hali ya umaskini wa kiuchumi na kielimu. Katiak nchi hizi watu wengi huishi kwa kutengemea kipato cha chini ya dola moja ya Kimarekani kwa siku. Hali ni mbaya zaidi katika sehemu za vijijini na mashambani ambako huduma za jamii ni duni sana. Upatikanaji wa maji safi na salama ni kitendawili, lakini pia huduma za afya ni duni na hazikidhi mahitaji ya wananchi wanaokaa huko.
Hata hivyo wananchi wengi wanaishi bila matumaini ya hari bora, maisha huwa magumu zaidi kila kunapoitwa leo. Wakati wananchi wa nchi zilizoendelea wakikabiliwa na matatizo ya kunenepeana kupita kiasi kutokana na kula kwa anasa na kukosa kiasi, wananchi wengi wa nchi zinazoendelea, hasa watoto mamilioni wanakufa kwa njaa. Kwa hakika adui mkubwa wa afya ya wananchi katika nchi zinazoendelea ni umaskini.
Muhammad Yunus katika kitabu chake cha “Creating a World without Poverty: Social Business and the Future of Capitalism” anasema kuwa “siku umaskini utakapoisha duniani, tutatakiwa kujenga majumba ya makumbusho ili kuonyesha vizazi vijavyo ubaya na athari za umaskini. Wajukuu zetu watashangaa na kushindwa kuelewa ni kwa njinsi gani umasikini uliweza kudumu miongoni mwa jamii ya watu. Lakini pia watashangaa sana kuona watu wengine wachache waliwezaje kuishi maisha ya anasa huku mamilioni ya watu wakiteseka”. Umasikini ni tatizo linalopingana na dhana ya demokrasia inayosema “wengi wape”.
Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya afya ya msichana na hali ya upungufu wa rasilimali inayofikia kiwango cha umaskini. Umaskini husababisha hali duni ya kiafya lakini pia hali duni ya afya husababisha umaskini na hali hii huwa sawa na mduara wa maisha.
Afya ya msichana hutegemea kwa kiasi kikubwa hali ya uchumi na kipato chake au kipato cha familia yake mahali anapokaa au kuishi.Umaskini husababisha msichana kukosa mahitaji yake ya msingi kwa ajili ya urembo, afya, elimu, maendeleo na uhuru. Katika hali ya umaskini, makazi, afya na lishe bora ya wasichana mara nyingi havizingatiwi wala kupewa kipaumbele, na rasilimali kidogo tu huwekezwa katika mahitaji ya kiafya ya wasichana wengi hasa katika nchi zinazoendelea.
Hali huwa mbaya pale wasichana wanapopata chakula kisichotosheleza mahitaji yao na huku wakiendelea kupoteza damu nyingi wakati wa hedhi kila mwezi. Upungufu wa damu na udhaifu wa mwili na akili huwa ni mambo yasiyoepukika katika kipindi hiki muhimu cha maisha.
Wasichana wanaokabiliwa na hali ya namna hii, huwa hawana uwezo mkubwa wa kupambanua mambo na hupoteza uwezo wa kiakili wa kukabiliana na masomo magumu kama vile masomo ya sayansi ambayo huwapa shida kubwa wawapo darasani.
Umaskini huwalazimisha wasichana wengi kutumbukia katika mambo ya hatari kama vile ngono zisizokuwa salama, biashara haramu kama vile kuuza na kusafirisha dawa za kulevya, biashara ya ngono, ndoa za utotoni na ajira mbaya yenye kipato duni licha ya kuwepo kwa hatari za kiafya. Mara nyingi wasichana maskini huwa ni wahanga wa ulaghai pamoja na unyanyasaji au ukatili wa kijinsia.
Mlundikano wa kazi na majukumu ya kifamilia ya kusaka mahitaji muhimu katika familia maskini, huongeza mzigo juu ya msichana na kumfanya asipate fursa za kuboresha afya yake kama vile kushiriki katika michezo, mazoezi na mapumziko ya kutosha. Katika familia masikini wasichana ndio wanaotembea umbali mrefu kila siku wakisaka maji kwa ajili ya matumizi ya familia nyumbani, ndio wazalishaji na waandaaji wa chakula cha familia na mambo mengine mengi ya lazima na muhimu.
Idadi kubwa ya wasichana wanaopata ujauzito katika umri mdogo inatokana na swala la umaskini, elimu duni juu ya utendaji wa miili yao au kutokupata elimu na huduma za afya ya uzazi. Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa asilimia 50 hadi 70 ya wanawake wanaopata ujauzito kwa mara ya kwanza maishani mwao katika nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara (Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi hizo) ni wasichana wadogo.
Tatizo la ujauzito katika umri mdogo huongeza hatari za kiafya kwa wasichana na pia huongeza mzigo wa umaskini katika familia, jamii, taifa na ulimwenguni kwa ujumla.
Wasichana wengi maskini hawapati ulinzi wa kisheria na kisera katika jamii zao. Pia wengi hawapati msaada wa hali na mali wa kuwawezesha kuepuka ngono zembe na hatarishi na hatari zingine zinazowakabili katika kipindi hiki. Hawapati elimu ya ujinsia, elimu ya afya na taarifa sahihi na za kutosha kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizoko katika barabara ya mafanikio yao.
Wasichana wengi wanaoishi katika familia maskini hukabiliwa na msongo wa mawazo, sononeko na mfadhaiko wa akili na wengi huishi na hali hii ya kuathirika kisaikolojia kwa muda mrefu. Wengi hupoteza hali ya kujiamini pamoja na uwezo wa kubuni mambo, lakini pia huwa ni watu wenye haya, soni au aibu sana.
Wengi hushindwa kujipangia vipaumbele vyao katika maisha na kupata hisia kuwa hawapewi hadhi katika jamii. Hali hii huwasababishia maumivu ya kihisia na maumivu ya mwili pia, na wengi hutumia muda wao mwingi kwenda hospitalini kuonana na madaktari kutokana na magonjwa ya kimwili ambayo chanzo chake ni maumivu na ugonjwa wa kihisia (Psychosomatic disorders).
Wasichana wengi wanaoathirika kisaikolojia hukabiliwa na wakati mgumu sana pindi wanapoolewa. Ndoa zao hukabiliwa na misukosuko mingi sana na wakati mwingine huwa ni ndoa zisizokuwa na amani, kuaminiana wala furaha na hatima yake huwa ni taraka. Lakini wengine wengi pia hushindwa kuolewa licha ya ukweli usiopingika kuwa wanatamani sana kuolewa.
Lakini pamoja na mambo hayo yote msichana anayekabiliwa na umaskini hana sababu ya kukata tamaa na kuacha mambo yaende kiholera au kutafuta njia za mkato kujinasua. Msichana anaweza kukabilianan na hali ya umaskini kwa mtazamo chanya, kwa kufanya kazi kwa bidii na kuanzisha miradi midogo midogo ya ujasiriamali wa kiuchumi kama vile kilimo cha bustani ya mbogamboga na matunda yanayokomaa kwa muda mfupi kama matikiti maji na mapapai au ufugaji wa kuku wa nyama na mayai.
Wasichana pia wanaweza kuuza vitabu, vipodozi salama na kujifunza kutengeneza na kuuza vyakula vyenye lishe kama soya, asali, mikate, jam ya karanga (peanut butter) au kuanzisha vitalu vya kibiashara vya miche ya miti au kuanzisha maduka ya uwakala wa huduma za kifedha kwa njia ya simu na miradi ya ushonaji wa nguo.
Miradi hii isiyohitaji mitaji mikubwa licha ya kuwapatia wasichana kipato, huwapa pia mazoezi ya mwili, mazoezi ya kukabiliana na changamoto za maisha na lishe bora kwa ajili ya afya na urembo wao. Msichana usikae kivivu ukisubiri mtu akupatie mtaji; vipaji ambavyo Mungu amekupatia kama msichana unaweza kuvitumia kwa njia ya ubunifu na kupata mtaji kwa njia halali.
Jifunze sitadi mbalimbali za maisha na kujisomea vitabu na majarida yanayoelimisha, hata kama huna elimu kubwa bado unayo fursa ya kupata elimu nje ya darasa itakayokuletea maendeleo endelevu. Mafanikio ya mtu hayategemei kiwango cha elimu ya darasani pekee, wapo watu wengi duniani wenye mafanikio makubwa lakini hawana kiwango cha juu cha elimu.
Usijiulize kuwa utafanya kazi au biashara gani kwa kuona kuwa kila huduma ipo tayari kwenye jamii, wewe anza na wazo lolote la kibiashara au ujasiriamali linalokufurahisha na ambalo unaamini una uwezo wa kulifanya. Boresha wazo hilo kiubunifu zaidi ya wengine na tumia talanta na nguvu zako zote zilizoko ndani yako kuliendeleza, nawe baada ya muda utaona mafanikio makubwa.
Tumia ujuzi ulionao kupata ajira au kujiajiri, kwani watu hawalipwi pesa kwa sababu wanajua mambo makubwa, ila wanalipwa kwa sababu wanatumia ujuzi walionao hata kama ni kidogo kufanya kazi na kuzalisha mali.
Usidharau kazi yoyote halali wakati huna kazi nyingine ya kukuingizia kipato katika maisha yako ya kila siku, hata kama wewe ni msichana unayefanya kazi za ndani (house girl), tumia vizuri nafasi na fursa hiyo uliyopata kwa ajili ya kujikomboa. Fanya kazi zako kwa umakini na kwa ufanisi mkubwa sawa na mtu aliyeajiriwa ofisini, jijengee tabia ya nidhamu ya kazi na nidhamu ya fedha.
Jiwekee akiba kwa kujinyima vitu vya anasa kama vile mapambo, vipodozi vyenye gharama kubwa, nguo za gharama kubwa, chips mayai, kuku wa kukaanga na simu za gharama ili akiba yako uitumie hapo baadaye kama mtaji wa biashara au kujisomesha. Kwa kufanya hivi utajitengenezea ajira ya uhakika wewe mwenyewe wakati wengine watakapokuwa wanalalamikia wazazi wao, ndugu zao, au serikali yao kwa kukosa kazi au ajira za kuwaingizia mapato.
Umaskini ni adui mkubwa wa afya na urembo wa msichana na mtu mwingine yeyote, lakini pia ni fursa ya kukuza uwezo wetu wa kukabiliana na changamoto za maisha ambao Mungu ameuweka ndani yetu. Kumbuka kuwa Mungu anatupatia maisha siyo utajiri wala umaskini, haya ni matokeo tu tunayoweza kuyasababisha au kuyarekebisha.
Hivyo basi msichana asikae kivivu na kusubiri mtu mwingine apambane na adui yake kwa niaba yake. Hakuna sababu ya kulalamika na kulaumu wengine kuwa hawakuletei maendeleo, kumbuka kuwa maisha ni mapambano na kila mtu anapambana kwa ajili ya maisha yake. Jitambue, uwe na maono ya mbali, fanya maamuzi sahihi na uchukue hatua.
Kila mtu amepewa na Mungu vipaji, fursa, nguvu, muda wa saa 24 kila siku na akili ya kukabiliana na adui umaskini. Ile dhana iliyozoeleka miongoni mwa wasichana wengi ya kuwategemea wavulana na wanaume kuwapatia pesa na mahitaji mengine, haiwezi kumkomboa mwanamke kutoka katika utegemezi na utumwa wa kiuchumi na kuleta fursa sawa kwa wote.
Ni vizuri wasichana wakatambua kuwa wavulana na wanaume wengi wanaowapatia fedha wasichana kwa ajili ya mahitaji yao, hufanya hivyo kwa muda tu na hawatakuwa tayari kuendelea kuwafadhili hivyo kwa muda wote wa maisha yao.
Upo wakati ambapo msichana hupoteza mvuto wake kwa wanaume kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata matatizo ya kiafya kama vile ugonjwa wa muda mrefu, kuwa na umri mkubwa, tabia zake zinapokuwa mbaya katika jamii au msichana anapopata ujauzito usiotarajiwa nje ya ndoa au sababu nyingine yoyote ile.
Wewe mwenyewe ni shahidi kuwa wavulana wengi huwatelekeza na kuwakataa wasichana wengi pale wanapowaeleza kuwa wana ujauzito wao. Kumbuka kuwa mambo mengi mvulana anayomfanyia msichana na vizawadizawadi anavyompatia ni sawa na kampeini za kisiasa.
Wavulana wengi hupenda kujifurahisha kingono na wasichana lakini hawako tayari kubeba majukumu na kuwajibika kwa matokeo yatokanayo na matendo yao. Katika kipindi cha kutelekezwa kama msichana hakujizoeza kuwa mzalishaji mali na mtu wa kujitegemea kimapato, atadhalilika na kupoteza thamani ya utu wake.
Wasichana wanaotamani kuziona siku zao za baadaye zikiwa na mafanikio makubwa ya kimaisha, kiafya na kupendeza, imewapasa sasa kusimama kwa miguu yao miwili na kupambana na changamoto zinazowanyima fursa ya kuamua mstakabali wao wa baadaye. Wasichana inawapasa sasa kutumia mapato na rasilimali zao binafsi na zile za familia zao kwa uangalifu na umakini mkubwa hasa kwa ajili ya mahitaji muhimu na ya lazima na kuachana na mahitaji ya anasa.
Ni jambo la busara kukumbuka kuwa Nuhu hakuingia katika safina wakati mvua ilipokuwa inanyesha, aliingia kabla mvua haijaanza kunyesha, fanya maandalizi, jenga msingi wa maisha yako ya baadaye sasa. Kuna wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna, chochote apandacho mtu ndicho atakachovuna.
Wewe kama msichana, jijengee tabia, mtazamo na mazoea ya kujitegemea kiuchumi. Usitegemee uzuri wa sura, umbo lako na urembo wako kuwa mtaji na kudharau kazi. Usitamani kuolewa na mwanaume tajiri ili ukaishi maisha ya kutanua bila kuzalisha, hili ni kosa la kiufundi katika maisha na siku moja utaona hasara ya kuweka matumaini yako kwa binadamu mwenzako ambaye hujui mwisho wa maisha yake utakuwa lini.
Hili ni jambo la kuzingatia hata kama msichana ni “star” au anatoka katika familia ya watu wenye uwezo kifedha kwani utajiri wa familia au “ustar” sio jambo linalodumu milele. Tofautisha umaarufu na mafanikio, wapo watu waliokuwa “mastar” zamani lakini leo ni watu wa kawaida, wapo watu waliokuwa matajiri zamani lakini leo familia zao ni familia za watu maskini. Wazazi matajiri na wanaume wenye uwezo wa kifedha wanaweza kufirisika au kufariki na miradi yao ikasambaratika wakati wowote. Hii ni kanuni ya maisha kuwa mabadiliko yanaweza kutokea wakati wowote na hakuna anayeweza kupinga mabadiliko.
Ni jambo la kushangaza kuona kuwa wasichana na wanawake wanoishi katika nchi maskini ndio wateja wakubwa wa vitu vya anasa, mapambo, vipodozi vingi visivyokuwa vya lazima na nywele za bandia kana kwamba hawana nywele. Na wakati mwingine inashangaza zaidi kuona kuwa wasichana hugharamia mahitaji yao ya anasa kwa fedha za kukopa au ada za shule walizopewa na wazazi wao maskini wanaojinyima kwa ajili ya kugharamia maendeleo ya elimu ya wasichana wao.
Mtu mmoja aliwahi kusema kwamba kama unataka kumfanya mtu awe mtumwa wako milele, mhamasishe kuifurahia na kujivunia minyiroro unayomfungia. Wafanyabiashara matajiri wanaoishi katika nchi zilizoendelea kwa njia za matangazo ya biashara, huwarubuni wasichana maskini wawe wateja wao wa kununua vitu visivyo na faida kwa kisingizio cha kwenda na wakati na biashara huria.
Kama mapato ya wasichana yatatumiwa kwa ajili ya mambo ya maendeleo ni wazi kuwa umaskini wa kipato utapungua miongoni mwa wasichana na afya zao za kimwili, kijamii na kiroho zitaimarika. Wasichana watakapofanya mapinduzi ya kweli katika jambo hili ndipo ule usemi usemao kuwa kumwelimisha mwanamke ni kuielimisha jamii nzima utakapokuwa na maana halisi na jamii itakuwa na hali bora kwa namna moja ama nyingine.
Tukumbuke kuwa jamii na nchi zetu licha ya kuwa na rasilimali za kutosha, tunaendelea kuwa maskini kwa sababu ya kusahau na kutokujua vipaumbele vyetu katika maisha. Tunasahau mambo tunayopaswa kukumbuka na tunakumbuka mambo tunayopaswa kusahau, tunaacha mambo tunayopaswa kufanya na tunafanya mambo tunayopaswa kuacha.
Siyo lazima kuishi maisha ya anasa ili tuonekane kuwa tuna mafanikio, kwani mafanikio yanaweza kuwa maisha rahisi na ya kawaida tunapoyaishi vizuri. Maisha ni kama mchezo wa karata, huwezi kushinda kwa sababu ya kuwa na karata nzuri bali unashinda kwa kucheza vizuri karata ulizonazo.
Wasichana wanahitaji kupata elimu ya kweli katika jambo hili ili kujikomboa dhidi ya utumwa na umaskini wa kifikra na umaskini wa kipato pamoja na kuimarisha afya zao. Wakati umefika kwa wasichana na wanawake wa Afrika kuwa wajasiriamali wadogo, wajasiriamali wa kati na wajasiriamali wakubwa bila kujali kuwa wametokea katika familia maskini au familia tajiri.
Wasichana ndio injini na maabara ya uhakika ya maendeleo ya jamii, ukitaka kujua hali ya maendeleo ya kweli ya jamii yoyote duniani, angalia hali ya wasichana, wanawake na watoto wa jamii hiyo.

🙉🙉🙉Usisahau kushare posti hii kuhusu (UMASKINI NA AFYA YA MSICHANA).👍 Share facebook, twitter, Google+ n.k bila kusahau WhatsApp! Share kote wenzio nao wasome💯✔

Unaweza kutafuta ndugu zako mliopotezana hapa Wanapatikana kirahisi kweli kwa sasa

👉SOMA ZAIDI HAPA...

Slide2-utotoni.GIF

.