Tafuta

.

Tafuta Mabesti wako wa zamani hapa Utawapata kwenye mtandao huu.

πŸ‘‰SOMA ZAIDI HAPA...

πŸ‘‰ NGUVU YA WAVUTI NA AFYA YA MSICHANAπŸ‘‡βœ”

NGUVU YA WAVUTI NA AFYA YA MSICHANA

Zipo faida nyingi za matumizi ya wavuti au mtandao (internet) katika maisha ya kila siku katika zama hizi za maendeleo, utandawazi, sayansi na teknolojia hasa pale dunia inapoendelea kuwa kama kijiji kimoja.
Kupitia wavuti wasichana kama ilivyo kwa watu wengine, wanaweza kupata habari, taarifa, elimu ya afya, kusoma kozi mbalimbali kwa njia ya masafa, kupokea na kutuma ujumbe kwa haraka, kupata marafiki, nafasi za kazi, kuagiza au kutuma bidhaa mbalimbali, kupata habari za biashara, habari za kibenki pamoja na vyanzo vya mikopo ya kifedha.
Pamoja na faida hizi za matumizi ya wavuti kwa watu wa malika mbambali, wavuti unazo hasara pia. Mbali na athari za kimaadili, matumizi ya wavuti yanaweza kutokeza hasara na athari za kiafya hasa kwa vijana. Wasichana wengi hasa wale wanaotoka katika familia zenye uchumi mzuri na wazazi wasomi, hukabiliwa na athari za kiafya, kijamii na kimaadili zinazotokana na matumizi mabaya ya wavuti endapo tahadhari hazitachukuliwa.
Kwa kawaida tovuti na mitandao mingi ndani ya wavuti hubeba habari nyingi nzuri na mbaya kwa vijana kulingana na umri wao.Uangalifu usipozingatiwa, tovuti hasa zile za mitandao ya kijamii, huwa sawa na maziwa mengi yaliyochanganywa na usaha kidogo kiasi kwamba huwa ni vigumu kwa vijana kutambua kipi ni maziwa na kipi ni usaha. Maamuzi sahihi na ukomavu wa kiakili huhitajika ili kutofautisha mambo yenye faida na yale yenye hatari katika mitandao au tovuti mbalimbali zinazopatikana katika wavuti hasa kwa vijana wa kike.
Kwa bahati mbaya sana wasichana wengi walio chini ya umri wa miaka 18, huachwa ili watumie wavuti wakiwa peke yao bila mwongozo wa wazazi au watu wazima. Unapofika wakati wa kupambanua mambo yenye faida na yale yenye hatari, wasichana wengi hutegemea uwezo wao wa kufikiri (common sense) na uzoefu wao wa utotoni katika kufanya maamuzi, jambo ambalo huwafanya washindwe kufanya maamuzi yenye manufaa.
Habari mbaya zaidi katika matumizi ya mitandao na tovuti nyingi katika wavuti kwa vijana hawa ni kwamba, uwezo wao wa kufikiri pekee hauwapi ulinzi na kinga ya kutosha dhidi ya nguvu hatarishi ya wavuti. Umri wao huwafanya wasiwe na uwezo wa kupambanua kinagaubaga kati ya mambo yenye usalama na yale yenye hatari.
Wasichana wengi wanaotegemea uwezo wao pekee huwa sawa na mbwa anapokutana na chatu mwenye njaa, mbwa hawezi kutumia uwezo wake kuepuka hatari inayomkabili kutoka kwa chatu mwenye njaa na uchu wa nyama.
Mitandao na tovuti nyingi katika wavuti zimetengenezwa kwa ustadi mkubwa kiasi kwamba hutokeza athari za kiafya kwa wasichana bila wao kujua kutokana na mambo yaliyomo ndani yake.Taarifa na habari zisizokuwa na msaada kwa maendeleo, mafanikio, afya na urembo salama, hupambwa vizuri katika mitandao ili kutimiza matakwa ya kibiashara.

Ujumbe, habari na taarifa katika wavuti
Ujumbe unaopatikana katika tovuti nyingi ndani ya wavuti zinaweza kuwa katika mfumo wa namna mbalimbali kama vile muziki, picha, barua pepe, habari za matukio, elimu, michezo ya tarakilishi, na mambo mengine mengi.
Wavuti hutoa uhuru mkubwa wa kuwasiliana na watu wengi unaowafahamu na usio wafahamu kitabia na kibnafsi hasa katika mitandao ya kijamii. Wavuti pia hutoa uhuru wa kufanya upendalo bila kuingiliwa wala kuchunguzwa bila kujali kuwa ni jambo jema au baya kwa ajili ya afya na usitawi wa kimaadili. Uhuru unaotolewa na wavuti katika swala la kupashana habari huwa zaidi ya uhuru unaotolewa na maisha ya kawaida ya kijamii, ambayo hudhibitiwa na kanuni za maadili, taratibu na maoni ya kitamaduni, kimila na kidini.
Msichana anapokuwa yeye peke yake na wavuti hana haja ya kufikiria kuwa watu wengine wanamuwaziaje juu ya taarifa, habari, picha, michezo au jumbe unazotuma au kupokea kupitia tovuti mbalimbali.
Wavuti pia hutoa nafasi ya kificha taarifa za siri ambazo huwafanya wasichana wengi wanaozifikia tovuti mbalimbali taratibu na kwa uhakika kuvutiwa na mambo ya ngono hatarishi kutokana na ukweli kuwa katika umri huu wasichana huwa wadadisi kuhusu ujinsia wao na tamaa ya ngono huwa na nguvu zaidi kuliko kipindi chochotekatika maisha yao.
Picha nyingi katika tovuti mbalimbali huwakilisha wasichana na wavulana katika mvuto wa kingono na urembo wa sura zaidi ya mvuto wa kitabia na kimaadili, hivyo huwavuta wasichana kupenda na kuiga mambo hayo. Mwanzoni wasichana hufikiri kuwa wanao uwezo wa kukinzana na nguvu hatarishi ya mtandao wa wavuti, lakini taratibu hujikuta wakiwa mateka wasio na nguvu ya kujinasua katika mtego ulioandaliwa kwa ufundi na ustadi mkubwa.
Kwa kutazama, tunabadilishwa taratibu ili kufanana na kile tunachokitazama, kukielekezea mawazo na kukiingiza akilini kupitia tovuti mbalimbali kila siku. Kwa kutambua hilo, ni vema wasichana wakajiwekea msimamo wa kinidhamu kwa ajili ya matumizi salama ya wavuti.

Urahibu wa wavuti (internet addiction)

Kutokana na mambo yaliyomo ndani ya wavuti kupambwa kwa umahili na kurahisisha mawasiliano, wavuti hutokeza tabia ya kutaka kuendelea kuutumia sawa na ulevi wa pombe au dawa zingine za kulevya.
Wasichana na vijana wadogo wanakabiliwa na hatari ya urahibu wa wavuti zaidi kuliko watu wazima. Ulevi huu huwafanya wale walioanza kutumia wavuti wapende kuendelea na kufikiria kuhusu wavuti wakati wote. Wavuti una tabia ya kuteka akili ya mtu na kumwongoza mtu kama upendavyo. Pale tabia ya kujidhibiti inapokosekana urahibu wa wavuti ni swala lisiloepukika kwa vijana.
Wapo watu wengine wenye ulevi huu wa wavuti ambao hupata hali ya kujisikia vibaya kihisia pale wanapokosa nafasi au fursa ya kutumia wavuti na wengine huona tovuti kama njia mbadala ya kupoteza hali ya kusongwa na mawazo au upweke. Wavuti huteka mawazo na akili kwa kiasi kikubwa.
Katika hali ya namna hii wasichana wenye ulevi wa wavuti kushindwa kupata usingizi wa kutosha kutokana na kutumia muda wa usiku wanapopata faragha katika kuangalia picha na kutumia wavuti hasa pale wanapomiliki simu za mkononi zenye mtandao wa wavuti (internet) au pale wanapokuwa na tarakilishi mpakato majumbani mwao zinazotumia modemu kuunganishwa na mitandao mbalimbali duniani.
Urahibu wa wavuti kwa vijana una uwezo wa kuathiri utendaji wa mwili kifiziolojia na utendaji wa akili kisaikolojia pamoja na uwezo wa kimasomo. Urahibu huu pia huharibu uhusiano wa kifamilia hasa pale vijana wanapoficha tabia yao ya matumizi yaliyokithiri na hatarishi ya wavuti ili wazazi wasitambue.
Hali hii pia hutokeza wasiwasi, hofu na msongo wa mawazo hasa kwa wasichana na kusababisha hali ya kupenda kujitenga au kutokuzingatia shughuli zingine muhimu za nyumbani na shuleni.
Jambo jingine linaloongeza msongo kuhusiana na urahibu wa wavuti ni matumizi makubwa ya kifedha ili kugharamia matumizi ya wavuti katika vibanda vinavyotoa huduma hii au kulipia gharama ya vifurushi (bundles) vya simu na modemu katika makampuni ya simu yanayotoa huduma hii.
Matatizo mengine ya kiafya kutokana na ulevi wa wavuti ni maumivu ya macho na kichwa yanayotokana na kuangalia mwanga wa skilini ya tarakilishi [computer] kwa kipindi cha muda mrefu. Maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo na maumivu ya maungio ya mikono pia yanaweza kujitokeza kutokana na kutumia tarakilishi kwa muda mrefu na kukaa kwa kipindi kirefu.
Wasichana wengi wanaotumia wavuti kwa muda mrefu, wamekuwa wakitumia dawa za maumivu ya kichwa mara kwa mara na wakati mwingine hutumia muda na rasirimali nyingi kupata huduma za afya ya macho ikiwa ni pamoja na kuvaa miwani. Uvaaji wa miwani ya ugonjwa wa macho kwa muda mrefu bila kupata ushauri wa daktari wa macho mara kwa mara si salama kwa afya.
Urahibu wa wavuti pia husababisha msichana atumie muda mwingi akiwa amekaa na kutokuufanyisha mwili wake mazoezi. Hii huleta athari za kiafya ikiwa ni pamoja na mwili kukosa ukakamavu, kunenepa ovyo, magonjwa ya moyo, ubongo na mapafu kutofanya kazi zake vizuri kutokana na upungufu wa kiasi cha hewa ya oksijeni kinachoingia mwilini wakati wa kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi ya mwili.
Hali hii pia inaweza kushusha kiwango cha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa na kuongeza hatari ya kupata magonjwa hatari ya saratani na kisukari.Wasichana wengi leo hukabiliwa na magonjwa haya yanayosababishwa na mtindo wa maisha usiofaa na hupoteza furaha na raha ya maisha mapema au baadaye sana.
 

πŸ™‰πŸ™‰πŸ™‰Usisahau kushare posti hii kuhusu (NGUVU YA WAVUTI NA AFYA YA MSICHANA).πŸ‘ Share facebook, twitter, Google+ n.k bila kusahau WhatsApp! Share kote wenzio nao wasomeπŸ’―βœ”

Jinsi unavyoweza kudumisha Amani na Upendo Kwa kujiunga na Kampeni ya Amani na Upendo

πŸ‘‰JUA ZAIDI...

kj.gif

.