MAPENZI NA AFYA

By, Melkisedeck Shine.

Kwa binadamu maisha ni kupata uzoefu wa mapenzi na kujifunza kila siku kuhusu mapenzi. Mapenzi ni hitaji la msingi la kila binadamu tangu siku ya kwanza ya maisha hadi siku ya mwisho wa maisha. Mapenzi ni hitaji la vitoto vichanga, wavulana na wasichana, wanawake na wanaume, wazee na vikongwe, matajiri na maskini, watawala na raia wa kawaida.
Maumbile yetu wenyewe yanashuhudia kuwa sisi ni viumbe tusioweza kutenganishwa na mapenzi. Mapenzi yako ndani ya bongo na akili zetu, katika moyo na roho zetu, katika damu na nyama zetu na katika kila chembechembe yenye uhai inayotengeneza miili yetu.
Maisha yetu hapa duniani yanachomoza kutoka ndani ya mapenzi na yanajengwa juu ya msingi wa mapenzi. Raha ya binadamu kuishi duniani inategemea sana dozi ya mapenzi yaani kupendwa na kupenda. Mapenzi ndiyo ikulu ya maisha ya mwanadamu, ndicho kitovu na nguzo ya maisha, ndicho kichocheo cha furaha na afya. Mapenzi sio ubunifu wa binadamu, asili na chimbuko la mapenzi ni ndani ya moyo wa Mungu aliyetuumba, Yeye ndie muasisi wa mapenzi.

Ni vigumu sana kutenganisha mapenzi na kusudi la kuumbwa kwetu. Hitaji letu la kupendwa na kupenda linatokana na maumbile yetu kuwa tumeumbwa kwa mfano na kwa sura ya Mungu. Kupendwa na kupenda ni zawadi ya thamani ambayo Mungu amewapatia viumbe – malaika, wanadamu, wanyama na mimea. Ni upendo wa dhati pekee unaoweza kutibu athari za msongo katika maisha ya binadamu. Upendo ndiyo chanjo inayomkinga binadamu asidhurike kutokana na upweke na sonona.
Ni kupitia mapenzi tu binadamu anatambua kuwa yeye ni mtu wa kuthaminiwa, kuheshimiwa na kutobaguliwa kwa misingi ya kiitikadi, kidini, kikabila, kijinsia, kitaifa au rangi ya ngozi yake. Mapenzi ndicho kichocheo cha amani, utulivu, raha, kuvumiliana na furaha. Ndani ya kila moyo wa binadamu imo shauku kwa ajili ya mapenzi, kila moyo una uwazi unaohitajika kujazwa kwa mapenzi kila siku.

Maana halisi ya mapenzi

Ingawa ni vigumu sana kueleza maana halisi ya neno mapenzi, kamusi ya Kiswahili sanifu iliyotolewa na Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili ya Dar-es-salaam, Tanzania inaeleza kuwa mapenzi ni ile hali ya kuingiwa moyoni na kuthaminiwa kwa mtu (au kitu) zaidi ya mwingine (au kingine). Mapenzi pia yanahusisha mambo ya mahaba au nyonda. [19]
Msomi mmoja alipokuwa akijaribu kueleza maana ya mapenzi yeye alisema kuwa mapenzi ni ile hali ya hisia inayoelekezwa kwa mtu au kitu kwa kutambua uzuri wake. [20] Ukweli wa mambo ni kwamba mapenzi ni zaidi ya hisia tu, huenda mbali hata kuhusisha vitendo na maneno kwa ajili ya ustawi wa anayependwa na anayependa.

Mapenzi yanaweza kugawanywa katika aina nyingi kutokana na mitazamo mbalimbali, ila hapa tunaweza kuyagawa mapenzi kama ifuatavyo:-

• Mapenzi ya Mungu kwa ulimwengu (watu na viumbe wengine)
• Mapenzi ya viumbe kwa Mungu.
• Mapenzi ya viumbe kwa viumbe wenzao.
• Mapenzi ya wanadamu kwa wanadamu wenzao.
• Mapenzi ya wanadamu kwa mali nk.

Mapenzi ya wanadamu kwa wanadamu wenzao

Mapenzi haya ndiyo yanayojulikana sana kwa watu wengi. Mapenzi haya pia yapo ya aina nyingi kama ifuatavyo:-

(1) Mapenzi bila masharti

Mapenzi haya yanamfanya anayependa ampende mwenzake kwa sababu ni binadamu mwenzake bila ya kujali vigezo vingine kama vile uzuri wa sura, makosa au kutazamia kupata faida.

(2) Mapenzi muambata/ mapenzi ya kiulinzi

Mapenzi haya yanatokana na hitaji la kulindwa kihisia linalopatikana katika kujumuika na kuambatana, kila mtu anahitaji kupendwa. Ili uwe mtu unahitaji mtu mwingine, wazazi wanahitaji watoto, watoto wanahitaji wazazi, ndugu huitaji ndugu na rafiki huitaji rafiki. Mapenzi haya yanatokana na hitaji la msingi la ulinzi wa kijamaa na kijamii.

(3) Mapenzi ya kirafiki

Msingi wa mapenzi ya kirafiki ni uhusiano mwema, ushirikiano na ulinganifu wa kiitikadi, mipango, mtazamo, kutunziana heshima, kushibana, kutiana shime, kusaidiana, kusifiana, kutendeana kwa upole na ukarimu. Marafiki ni watu muhimu kwa ajili ya afya zetu.
Marafiki wa kweli huwa na upendo wa dhati kwa rafiki zao wakati wote bila kujali shida na raha. Urafiki hauna mipaka ya umri au jinsia lakini tahadhari inapaswa kuchukuliwa na wasichana wanaokabiliwa na uamuzi wa kuwa na marafiki wa jinsia tofauti. Wakati wa balehe msichana anapoandamana na mtu wa jinsia tofauti ampendae kimahusiano, tamaa yake ya kingono inaweza kuamshwa. Huu ni ukweli wa kibaiolojia unaotokana na maumbile yanayohusiana na baiokemikali za mwili. Urafiki wa jinsia tofauti huhitaji ukomavu na udhibiti wa hisia. Wasichana na vijana wenzao wa kiume mara nyingi hukosa uwezo huu na urafiki wao huishia katika ngono japokuwa mwanzoni wasichana hujiamini na kuonyesha msimamo.

(4) Mapenzi ya mahaba

Mapenzi ya mahaba au huba yanaweza kuwa mapenzi ya dhati au mapenzi ya bandia na ya uongo. Mahaba pia yaweza kuwa matamanio ya kimsisimuko yatokanayo na mhemko wa muda mfupi uliojengwa juu ya urembo na kupendeza kwa sura. Mapenzi bandia mara nyingi hutokeza athari za afya ya mwili, akili na roho hasa kwa wasichana.Hii hutokea pale vijana wanaposhindwa kutofautisha kati ya mapenzi na ngono.
Ngono kwa wanaume na wanawake waliokomaa kihisia na wenye nia na mapenzi ya dhati katika ndoa, ni njia yenye nguvu sana ya kuonyesha mapenzi ya mahaba. Mahaba ya dhati kwa sababu halali, kwa wakati muafaka, katika umri sahihi, kwa lengo na mtazamo sahihi unaotokana na uchaguzi bora, hudumisha afya na ustawi wa wahusika. Katika ndoa halali, ngono ni njia ya mawasiliano ya kimahaba inayotoa ujumbe kwa kila mhusika kuwa mwenzake ni wa muhimu kwa ajili ya kuambatana kwa maisha yao yote yaliyobaki.
Ni jambo lisilopingika kwamba mapenzi ya mahaba ya dhati yanahitaji ukomavu kihisia na kiakili. Vijana wadogo ambao hawajakomaa kimwili na kiakili kamwe hawawezi kuwa na mapenzi ya mahaba ya dhati. Mapenzi ya mahaba katika umri mdogo mara nyingi hujengeka katika sifa na vigezo vinavyopita na kutoweka upesi kama vile uzuri wa umbo, rangi, sura ya mtu, mali au sifa ya umaarufu. Vitu hivi vinapotoweka mapenzi nayo hutoweka, hii ndiyo sababu ndoa za vijana wanaooana katika umri mdogo huvunjika mara kwa mara.

Je, Mapenzi yanaweza kuumiza?

Mapenzi ya mahaba yanaweza kumaanisha uhuru au utumwa, yaweza kuwa matamu kama tunda la tofaa (Apple) au makali kama pilipili. Yaweza kuwa matamu kama asali pia yaweza kuwa machungu zaidi ya shubiri. Mapenzi yanaweza kuambatana na hali ya kukosa hamu ya chakula, kukosa usingizi, kujiua au kunywa sumu pale umpendaye anapokuacha. Kuachwa au kutelekezwa na mtu unayempenda, kunaweza kuleta maumivu makali ya kihisia moyoni.
Mapenzi pia yanaweza kuharibu masomo na mipango ya maisha, yanaweza kuharibu afya na mahusiano bora na wazazi. Maumivu hayo mara nyingi hutokea pale lengo na makusudi ya mapenzi yanapokuwa batili. Maumivu yanaweza kuibuka pale mmoja wa wapenzi anapotaka matwakwa yake yatimizwe na kujinufaisha kibinafsi. Na mara nyingi mapenzi hayo ya kimahaba huwa ni yale yaliyochipua harakaharaka na kuingiwa bila tafakari ya kutosha.
Mapenzi muambata na mapenzi ya kirafiki pia yanaweza kusababisha maumivu kwa vile wapendwa wetu sio wakamilifu kwa asilimia mia moja. Wazazi wanapokanya, kukemea au kutoa adhabu kwa watoto wao mara nyingi vijana huumizwa sana kihisia. Vijana imewapasa kuziona adhabu halali zinazozingatia ubinadamu kuwa ni sehemu ya mapenzi. Wazazi wanaompenda kijana wao kwa dhati hawawezi kamwe kunyamaza wakati wanajua hatari inayomkabili kijana hapo baadaye. Hakuna kitu kingine mbali na upendo kinachowasukuma wazazi au walimu kumkanya kijana.

Faida za kupenda na kupendwa

Je, ni mtu gani hapa duniani asiyependa kupendwa? Kupendwa ni mojawapo ya mafaniko ya binadamu. Roho ya mtu ikikosa mapenzi hata kwa dakika tano roho hufa sawa na mwili unavyokufa ukikosa hewa ya oksijeni. Mapenzi ni muhimu kwa afya sawa na chakula au maji. Mtu mwenye afya ni lazima anayo akiba ya mapenzi moyoni mwake. Akiba hii ikiisha kabisa, na kuwa 0% maisha yanapoteza umuhimu na maana yake, hapo ndipo mtu anapotamani kufa kuliko kuishi.
Mapenzi yana uwezo wa kuponya magonjwa ya msongo, maumivu ya kichwa au mwili na kuleta utulivu wa kihisia. Takribani asilimia 60-70 ya magonjwa yanayowasumbua watu wengi hutokana na msongo wa mawazo au hali ya kusononeka. Mapenzi na kuwahudumia wengine kwa upendo hupunguza kasi ya kuzeeka na kusaidia katika uponyaji wa magonjwa ya moyo na akili. Mtu mwenye mapenzi mema mwili wake huzalisha vichocheo kama vile ‘Dehydroepiandrosterone (DHEA)’ na ‘Endorphins’ ambavyo huchangamsha mwili na kuongeza kinga ya mwili pamoja na kupata usingizi mzuri.
Mapenzi mema pia hupunguza kiwango cha lehemu (cholesterol) mbaya mwilini, husaidia katika uponaji na kuzuia vidonda vya tumbo, ugonjwa wa kiharusi (stroke) na huongeza uwezo wa mtu kukumbuka mambo. Ieleweke kuwa mapenzi mema ya mahaba ni yale yanayopatikana ndani ya ndoa halali pekee na si vinginevyo.

[kitendawili Kwako] 👉Ina paa, madirisha na milango

Endelea kusoma makala hizi zifuatazo;

a.gif UREMBO NA MAVAZI YA MSICHANA

Ingawa ni vigumu kueleza kinagaubaga maana halisi ya neno urembo, naweza kusema kuwa urembo ni utumiaji wa mapambo, manukato, marashi, uturi, mavazi na rangi ili kuremba na kuongeza nakshi na umaridadi katika mwonekano, sifa na viwango vya ubora wa msichana au mwanamke kwa lengo la kuvutia au kufurahisha hisia (za kuona, kunusa au kugusa) za mtu mwingine atakayekutana naye… soma zaidi

a.gif MAMBO YANAYO BORESHA AFYA YA MSICHANA

Wasichana wanahitaji mlo kamili na chakula kingi zaidi ya wanawake watu wazima wenye uzito sawa na wao. Katika kipindi hiki cha makuzi na kupevuka msichana huhitaji viini lishe vya kutosha. Katika kipindi hiki protein, madini ya chokaa, chuma na zinc huhitajika mara dufu. Vitamini, wanga na mafuta pia huhitajika kwa wingi.
Kupoteza damu wakati wa hedhi na mchakato wa kukua huongeza mahitaji ya madini chuma katika mwili wa msichana. Msichana anahitaji kula chakula chenye asili ya mimea, kula matunda na maji ya matunda (juice) kwa wingi. Nafaka na mboga za majani, vyakula vitokanavyo na mizizi kama karoti, viazi na vyakula vingine ni muhimu sana.
Wasichana inawapasa kuepuka vyakula visivyo na viini lishe vya kutosha, vyenye sukari nyingi, chumvi nyingi pamoja na mafuta mengi ambavyo huandaliwa kwa harakaharaka au kufungashwa viwandani (junk foods). Vyakula vya namna hii, vinaweza kusababisha matatizo ya kiafya kama vile kutoa kinyesi kikavu, unene wa kupindukia, kisukari, shinikozo la damu, uchovu wa mwili wa mara kwa mara, uvimbe wa maungio na vifundo vya mwili pamoja na magonjwa ya figo… soma zaidi

a.gif JINSIA NA MAHUSIANO KWA MSICHANA

Jinsia ni ile hali ya kuwa mtu wa kiume au wa kike. Ni swala la mahusiano kati ya wanaume na wanawake yanayoamuliwa na mila na desturi za jamii husika. Mahusiano haya ya kijinsia hutoa mgawanyo wa haki, wajibu na majukumu kwa jinsia hizi mbili. Kwa maana hiyo siyo maumbile ya kibaiolojia ya viungo vya uzazi yanayoamua jinsia ya mtu.
Watu huzaliwa wakiwa na jinsi ya kike au kiume na kutokana na malezi pamoja na mgawanyo wa majukumu ya kijamii, huwa wanaume au wanawake. Majukumu ya kijinsia hutofautiana kati ya nchi moja na nyingine, kati ya kabila moja na jingine. Katika mahusiano bora ya kijinsia ni lazima haki za kijinsia ziheshimiwe. Msichana anayo haki ya kutawala mwili wake mwenyewe na kuamua kuhusu mahusiano yake na wengine kwa namna ambayo inadumisha afya na ustawi wake kwa mjibu wa sheria na taratibu za jamii… soma zaidi

wadogo.gif

a.gif Kampeni ya utunzaji wa wanyama pori

Kampeni hii ilianzishwa na Melkisedeck Leon Shine mwaka 2018.
Lengo la kampeni Hii ni kuhamasisha watu kutunza wanyama pori kwa manufaa yao ya sasa na kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Kampeni hii inaamini kuwa wanyama pori wakitunzwa vizuri wanaweza kuwa msaada kijamii, kiuchumi na kimazingira kwa kizazi hiki na kizazi kijacho… soma zaidi

a.gif Je, matokeo ya kupima na kukutwa huna virusi vya Ukimwi ni yapi?

Kwa kawaida mtu anapoamua kwenda kupima mara nyingi anakuwa na sababu za kumfanya ahisi kuwa au kutokuwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Kwa hiyo mtu akipata jibu kuwa hana maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, i itabidi ajiulize huo wasiwasi ulitokea wapi.
Pale mtu anapojua ni kitu gani kilimfanya aende kupima, ni vyema mtu huyo kukaa mbali / kuacha kurudia hilo jambo au tabia i iliyomweka katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Kwa mfano, kama alifanya ngono na mtu zaidi ya mmoja na kwa nyakati zote hakutumia kondomu. Baada ya kupima, mtu huyu anatakiwa aache tabia ya kuwa na wapenzi wengi na pia awe anatumia kondomu kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Ni muhimu kuchukua tahadhari zote i ili kujikinga na maambukizi ya Virusi na UKIMWI na UKIMWI… soma zaidi

a.gif Mahusiano ya kimapenzi kati ya msichana mwenye umri mdogo na watu wazima

Inawezekana kwa msichana mdogo kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwenye umri mkubwa. Hata hivyo uzoefu umeonyesha kwamba uhusiano kama huo mara nyingi unakuwa mgumu. Kwanza kabisa ni suala la upevu wa akili na uwiano wa jinsi ya kufurahia maisha… soma zaidi

a.gif Mapishi ya Biriani Ya Kuku Wa Kuchoma Wa Tanduri

Mchele - 4 vikombe.. soma zaidi

a.gif Je, kuna njia salama ya kutoa mimba?

Hatari inategemea na mazingira ambapo mimba inatolewa. Kama ni hospitalini na i inatolewa na mtaalamu aliyesomea na kama mazingira na vifaa ni safi, uwezekano wa kutoa mimba salama ni mkubwa. Lakini, hata katika mazingira hayo, shida zinaweza kutokea… soma zaidi

Usipitwe na Nafasi za kazi kwa leo

<<Bofya HAPA kujua zaidi>>

.

Website na, Melkisedeck Leon Shine | Tembelea website nyingine Hapa>>.