Tafuta

👉 MAOMBI👇✔

MAOMBI

Somo: Zaburi 107

Kuweza kumwomba Mungu wa mbinguni ni fursa tuliyonayo ya kipekee sana. Ni fursa ambayo yeye Mungu ameitoa kwa kila mtu aliye mnyenyekevu, na ambaye anatambua kuwa yeye Mungu ndiye aliyekifanya kila kitu kilichopo duniani. Kuomba/kusali kunaweza kukaonekana kuwa ni kitu kigumu. Sababu ni kwamba, kuna mtengano ulio mkubwa sana kati ya Muumba aliye mbinguni na vitu alivyoviumba vilivyoko katika dunia.

Hata hivyo Mungu ameweka wazi wakati wote kuwa, yupo tayari kukaribiwa na watu ili waseme Naye, kama wana uelewa ulio sahihi mioyoni mwao, na kama wako tayari kulikubali Neno lake:
“BWANA asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu.…lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka atetemekaye asikiapo neno langu” (Isaya 66:1, 2).

Kwa hiyo tuna ahadi ya kwamba, Mungu atatuitikia kama tukimjea kwa unyenyekevu wa kweli.

Tunaweza tukafikiri kuwa sio rahisi kusema moja kwa moja na Mungu. Na kweli, katika nyakati za Agano la Kale, watu mara nyingi waliogopa sana walipokuwa wanajisikia wapo katika ‘uwepo’ na Mwenye-Enzi yote. Wana wa Israeli, kwa mfano, walipotoka Misri, utukufu wa Mungu uliposhuka katika Mlima Sinai, kila mmoja wao, akiwepo Musa, walitetemeka na watu kusimama mbali (Kutoka 19:17-20 na 20:18-21).

Mungu alikuwa akiwakaribia watu wake, taifa lake, lakini utisho wa Ukuu waliouona uliwafanya wajione hawawezi kuwa na ukaribu na Utakatifu wa uwepo wake. Pengine hata sisi tungejisikia hivyo hivyo. Waliogopa kiasi cha kumwomba Musa awe mtu wao ‘wa-kati’ kati yao na Mungu; kiunganishi chao; mpatanishi. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwamba, baada ya hapo Mungu aliwasiliana na Israeli kupitia kwa mtu-wa-kati.

Hema la Kukutania lilipojengwa kuwa mahali pa kuabudia nyikani, Utukufu wa Mungu uling’aa juu ya Sanduku la Agano katika sehemu takatifu zaidi ya Patakatifu (Patakatifu pa Patakatifu). Hakuna mtu aliyekuwa akiruhusiwa kuingia hapo penye ‘uwepo wa Mungu’, zaidi ya Kuhani Mkuu, mara moja kwa mwaka, katika Siku ya Upatanisho. Katika siku hiyo Kuhani Mkuu alizikiri mbele ya Mungu dhambi zote za taifa la Israeli, na kwa vizazi vingi huu ukawa ndio mfumo wa Upatanisho kwa Wayahudi wote.

Walikuwa ni watu wa kumkaribia Mungu kwa namna aliyoiweka, na hili lilikuwa ni jambo lililowekwa kuwaongoza kwenye ‘kazi za Yesu’, ambaye ni ‘Mpatanishi’ kwa ajili ya wafuasi wake. Alipopaa mbinguni, aliwekwa awe ‘Kuhani Mkuu aliye mwaminifu’ kwa ajili ya wanaomfuata wote, wawe Wayahudi au wasiwe, mradi wamebatizwa ‘katika Kristo’.

Mtu wa kawaida anaweza kuongea na Mungu
Swali: Hakukuwa na njia nyingine ya kumjea Mungu ila kwa kupita kwa kuhani wa Kiyahudi au kwa kutoa sadaka? Ni vipi kwa:
• Watu walioishi kabla hakujawa na taifa la Israeli?
• Watu ambao hawakuwa Wayahudi?
• Watu ambao walitaka tu kumwomba Mungu msaada?
• Wayahudi baadaye walipokuwa wakiishi katika nchi za kigeni?

Je, hawakuwa wakiweza kusema na Mungu moja kwa moja? Tunajua kutokana na kusoma kwetu Biblia zetu na mifano mingi sana ya maombi kwa Mungu wa mbinguni kuwa, Mungu wakati wote huwa anayasikia maombi ya watu.

Kwa mfano, tulisoma katika Mwanzo 24 kumhusu mfanyakazi wa Ibrahimu aliyeomba afanikiwe kwenye safari yake ya kumpatia Isaka, mwana wa Ibrahimu, mke. Tunaona namna mtumishi huyo alivyomshukuru Mungu maombi yake yalipojibiwa. Tunaweza kusoma pia katika Ayubu 42 jinsi Ayubu alivyoomba kwa ajili ya marafiki zake, hapo Mungu alipomponya kutoka katika ugonjwa wake wa kutisha.

Hana, mama yake Samweli alimwomba Mungu kwa sababu alikuwa tasa (1 Samweli 1 na 2), na Danieli, akiwa mateka Babeli, na madirisha katika chumba chake yakiwa yamefunguliwa kuielekea Yerusalemu ilipo, alipiga magoti mara tatu kila siku, “Akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo” (Dan. 6:10).

Tena, tunayo dua ya mfalme Sulemani akimwomba Mungu ili ayasikie maombi ya wageni, akisema:
“Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako, (maana watasikia habari za jina lako kuu, na za mkono wako ulio hodari, na za mkono wako ulionyoshwa); atakapokuja na kuomba kuielekea nyumba hii; basi, usikie huko mbinguni makao yako, ukatende kwa kadri ya yote atakayokuomba mgeni huyo; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe….” (1 Wafalme 8:41-43).

Vipi juu ya watu hao wote, wanaomwitia Mungu wanapokuwa katika shida? Atawasikia hata kama mara nyingine wanakuwa wamemsahau? Jibu ni ‘ndio’, kama ni wakweli na wanyenyekevu na wana moyo wa toba. Hebu tuiangalie mifano tuliyopewa kwenye Zaburi ya 107:
• Wenye njaa na kiu wanalishwa (ms. 5,6).
• Wale wanaomuasi Mungu, lakini baadaye wakatubu, wanaponywa na shida zao (ms. 13).
• Mungu anawasikia wale ambao ‘wameyakaribia malango ya mauti’ (ms. 18).
• Mungu anawasikia wale ambao wako katika hatari ya kuzama majini (ms. 28).

Fundisho hili limejumlishwa kwenye msitari wa 6: “Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, akawaponya na shida zao”.

Tutaongeaje na Mungu?
Katika Agano Jipya wakati wa huduma ya Yesu, Bwana Yesu anatuambia juu ya ‘mtoza ushuru’ na ‘mdhambi’; watu ambao walidharauliwa na Wayahudi wengi. Mdhambi alisimama mbali, wala hakuthubutu kuinua macho yake, bali alijipiga-piga kifua chake na kuomba, “Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi” (Luka 18:13).

Yesu anasema, mtu kama huyo alisikiwa na Mungu kwa maana alijinyenyekeza, tofauti na mafarisayo, ambao walijiona ‘wa maana’ sana kwa jitihada zao wenyewe za kuishi maisha mazuri.

Kwa hiyo tunaona ya kwamba, Mungu amewawekea watu wakweli, popote pale walipo, fursa ya kumkaribia kwa njia ya sala. Ni hivyo ilivyo hata wakati huu, na tunaweza kujifunza mengi sana kutoka katika mifano hii ya Kibiblia. Mtu yeyote yule, awe mwanamume au mwanamke, anayemtafuta Mungu na kujifunza Neno lake, kwa vyovyote ataona haja ya kumwomba.

Mungu anavijali viumbe vyake vyote na atasikia kila ombi lililo la kweli. Mtu anayemtafuta Mungu atapenda kumsifu na kumwabudu kwa dhati; kumshukuru kwa mibaraka yake ya uzima na hasa kwa mbaraka wa Neno lake kwake, Biblia.

Anapokuwa amejifunza juu ya dhambi, atatamani kuzikiri dhambi zake kwa Mungu, na Mungu atamsikia. Lakini kuna jambo moja la kutambua. Mungu atasamehe tu dhambi kwa njia aliyoiweka; nayo ni kwa kupitia katika dhabihu ya Bwana Yesu Kristo, na hili linahitaji muumini awe amebatizwa kwanza.

Akida wa Kirumi, Kornelio, alikuwa akifanya maombi yaliyokuwa yakifaa sana. Tunaambiwa, alikuwa: “Mtu mtauwa, mchaji wa Mungu yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima” (Matendo 10:1).

Maombi ya Kornelio yalisikiwa, na Mungu akamtuma mtume Petro kumkamilisha kimafundisho, na baada ya hapo kumbatiza katika Jina la Bwana Yesu (utakisoma hiki kifungu chote mbeleni).

Ombi la muhimu kuliko yote kwa ajili ya mtu anayejifunza kumhusu Mungu, pengine ni lile linalopatikana katika Kitabu cha Zaburi 119:
“Unifumbue macho yangu, niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako” (ms:18).

Tunapaswa wote kumwomba Mungu abariki kusoma kwetu na kujifunza kwetu Neno lake.

Mungu atajibu?
Kwa lolote tunalotaka, tunapaswa kulileta kwa Mungu kwa njia ya maombi:
 Lakini, atajibu?
 Anajali wakati wote?
 Anaweza wakati wote kufanya linalotakiwa?
Haya ni maswali ya kufaa, na yana majibu ya hakika kwenye Biblia.

Kusali sio fursa kwa ajili yetu kumwekea Mungu mahitaji yetu yote, ili atupe vitu vyote tunavyopenda kuwa navyo. Kuomba ni sehemu tu ya ibada yetu. Kunatupa nafasi ya kuyafikiria kwanza mambo mbele ya Mungu anayetupenda, na anayetutakia kilicho bora zaidi. Mtume Paulo anasema:
“Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu” (Wafilipi 4:6).

Tunapaswa kuomba kwa imani, lakini ni lazima kuomba kulingana na mapenzi ya Mungu, ili mapenzi yake yatimie. Hili lina maana ya kusoma Biblia ili kuyajua mapenzi yake yalivyo na kusudi lake, na sio kuomba kwa ajili ya vitu tunavyoambiwa hatuwezi kuvipata. Tukumbuke pia kwamba, Mungu mara nyingine anajibu maombi kwa kututaka tusubiri, mara nyingine kwa muda mrefu.

Ibrahimu aliomba, lakini ilimbidi asuburi kwa miaka mingi kumpata mwana ambaye Mungu alikuwa amemwahidi kumpa. Mara nyingine Mungu anatujibu kwa kukataa; kwa kuacha kutupa kile tunachomuomba. Yeye anajua lililo bora zaidi kwetu, kuliko tunavyojua wenyewe linalotufaa. Lakini kamwe haachi kutujali na kutupenda. Kwa wenye-haki, wakati wote, “Masikio yake hukielekea kilio chao” (Zab. 34:15).

Kujifunza kusali
Tunajifunza kusali kwa namna ile ile tunavyojifunza kuongea; kwa kuanza kujifunza kwa wengine, na kujaribu baada ya hapo kufanya kama wao. Kwa hiyo inafaa twende kwenye Biblia kwa ajili ya mifano. Biblia imejaa maombi. Kwenye Zaburi, kwa mfano, kuna maombi kama 150 tofauti-tofauti tunayoweza kujifunza vitu ndani yake. Kuna mengi pia ya kujifunza katika maombi ya manabii na Yesu na wanafunzi wake.

Kama tukiyasoma Maandiko kila siku, tutajenga mwelekeo wa kiakili unaoweza kumpendeza Mungu. Tutajengeka kwa namna tunavyofikiri, na tutajengeka kwa namna tunavyosema na Mungu. Tunaweza pia kuwafanya wengine wawe kama sisi kwa kuomba kwetu: kama katika kumshukuru Mungu kabla ya kula, au kwa kupiga magoti pembeni mwa kitanda kabla hatujalala.

Tunaweza kuomba wakati wowote ule, mara nyingi kwa kadri tunavyopenda: tukiwa nyumbani au safarini au kazini au shambani. Yesu alikuwa akipenda kuondoka kidogo peke yake asubuhi-subuhi, kwenda mahali palipotulia, kuomba.

Lakini tunaweza pia kuomba katika mkasa wowote, kama ambavyo tunavyoweza kumshukuru Mungu kwa mambo ambayo yanakwenda vizuri na kwa mibaraka yetu yote. Watu wengi wa-imani wanaona vizuri kuwa na muda maalumu wa maombi ya kibinafsi, mara nyingi asubuhi na jioni. Hili ni jambo jema, lakini kamwe tusipuuzie fursa yoyote kuongea na Bwana.

Maombi ya muumini aliyebatizwa
Tulitaja awali katika somo hili kuwa, kuna jambo la kipekee kuhusu maombi kwa wale waliobatizwa katika Kristo. Kama vile ambavyo Kuhani Mkuu alivyokuwa mpatanishi kwa ajili ya Waisraeli, ndivyo ambavyo Yesu Kristo alivyo Mpatanishi kwa ajili ya wafuasi wake wote wa kweli. Uhusiano wa kipekee na Mungu kupitia kwa Mwanawe unaokuwepo, ni kitu kwa ajili yako kilichowekwa ukitazame kwa furaha kama, kwa neema ya Mungu, umebatizwa.
Ina maana kuwa, unapozikiri dhambi zako kwa Mungu kwa Jina la Yesu, Mungu anakusamehe dhambi zako, na hili lina maana ya kwamba hatazikumbuka tena.

Yesu Kristo ni Mpatanishi kwa waumini waliobatizwa

Dhambi za Waisraeli hazikuondolewa walipokuwa wakitoa sadaka za wanyama. Mshahara wa dhambi ni mauti. Wanyama hawakuwa na akili kuhusiana na dhambi, na wasingeweza kuifia dhambi; kutoa damu yao wenyewe. Imeandikwa katika Waebrania 10:4 kuwa: “Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi”.

Lakini Yesu alikuwa ndiye sadaka kamilifu kwa kuwa, kwa damu yake mwenyewe alijitoa bila ya dhambi (Waebr. 9:12). Kwa hiyo, wale wanaobatizwa katika Yesu wana:
“Kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu”, ambaye, “Alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi” (Waebr. 4:14, 15).

Yesu Kristo ni Kuhani Mkuu kwa ajili ya waumini waliobatizwa

Ubatizo wa kweli wa Kikristo ni wa muhimu sana. Una matokeo ya kuziosha dhambi zetu (Matendo 22:16) na tunapokuwa tumebatizwa, ndipo tunapoweza kumkaribia Mungu kupitia kwa Yesu Kristo, tukijua ya kuwa: “Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote” (1 Yoh. 1:9). Ndipo tutakapoweza kutumia maombi Bwana Yesu aliyowafundisha wanafunzi wake, akisema:
“Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe siku kwa siku riziki yetu. Utusamehe dhambi zetu; kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni, lakini tuokoe na yule mwovu” (Luka 11:2-4).

Haya yatakuwa ni maombi ya maana sana kufanya kwa kuwa, mwenye kheri ni yule: “Aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa yake” (Zaburi 32:1).

Muhtasari:
1. Ni lazima kumkaribia Mungu kwa namna aliyoiweka.
2. Mungu atayasikia maombi ya wote walio wanyenyekevu na wakweli.
3. Tunapaswa kutoa shukrani na sifa, kuzikiri dhambi zetu na kumwomba Mungu atuongoze na kutubariki.
4. Ni wajibu wetu kujifunza kuomba kwa ajili ya vitu sahihi na kwa namna iliyo sahihi.
5. Kuomba ni fursa tuliyopewa ya bahati sana na ni mbaraka mkubwa. Ni lazima tuombe mara kwa mara.
6. Baada ya kubatizwa tunaweza kuomba kupitia kwa Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya kusamehewa dhambi zetu. Ndipo Mungu atakapokuwa Baba yetu, na kuwa Mungu wetu.

Vifungu vya kusoma: Matendo 10; Zaburi 51, 102; Luka 18:1-14.

Kujifunza kwa moyo: Wafilipi 4:6
“Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu” (Wafilipi 4:6).

🙉🙉🙉Usisahau kushare posti hii kuhusu (MAOMBI).👍 Share facebook, twitter, Google+ n.k bila kusahau WhatsApp! Share kote wenzio nao wasome💯✔

Umerahisishiwa kutafuta mliopotezana Ni rahisi sana kutafuta wale uwapendao

👉SOMA ZAIDI HAPA...

rafiki.gif

.