Tafuta

Umerahisishiwa kutafuta mliopotezana Ni rahisi sana kutafuta wale uwapendao

πŸ‘‰SOMA ZAIDI HAPA...

πŸ‘‰ JINSIA NA MAHUSIANO KWA MSICHANAπŸ‘‡βœ”

JINSIA NA MAHUSIANO

Jinsia ni ile hali ya kuwa mtu wa kiume au wa kike. Ni swala la mahusiano kati ya wanaume na wanawake yanayoamuliwa na mila na desturi za jamii husika. Mahusiano haya ya kijinsia hutoa mgawanyo wa haki, wajibu na majukumu kwa jinsia hizi mbili. Kwa maana hiyo siyo maumbile ya kibaiolojia ya viungo vya uzazi yanayoamua jinsia ya mtu.
Watu huzaliwa wakiwa na jinsi ya kike au kiume na kutokana na malezi pamoja na mgawanyo wa majukumu ya kijamii, huwa wanaume au wanawake. Majukumu ya kijinsia hutofautiana kati ya nchi moja na nyingine, kati ya kabila moja na jingine. Katika mahusiano bora ya kijinsia ni lazima haki za kijinsia ziheshimiwe. Msichana anayo haki ya kutawala mwili wake mwenyewe na kuamua kuhusu mahusiano yake na wengine kwa namna ambayo inadumisha afya na ustawi wake kwa mjibu wa sheria na taratibu za jamii.
Wasichana kama watu wengine ni viumbe ambao wanahitaji kujumuika ili kukamilisha ubinadamu wao. Kila mtu anahitaji mahusiano kwa ajili ya afya na ustawi wake.Upo wakati ambapo wasichana wanahitaji mahusiano na wavulana, lakini ili mahusiano ya wasichana na wavulana yawe salama na yanayodumisha afya, ni lazima msichana awe na stadi za maisha zinazo muwezesha kufikia azima hiyo. Stadi za maisha ni uhodari au ufundi wa kitabia unaotakiwa ili kukabiliana na matakwa ya maisha ya kila siku kwa njia iliyo salama. Ni uwezo wa kutumia maarifa, vitendo, ujuzi, mtazamo, itikadi na taarifa zinazomwezesha mtu kukabiliana na mazingira mbalimbali ili kupata mafanikio maishani. Kuna aina nyingi za stadi za maisha, baadhi ya stadi zenye manufaa kwa msichana ni pamoja na:-
Stadi za kazi: mfano ushonaji, upishi, ufugaji wa kuku, biashara nk. Stadi za kazi humsaidia msichana kumudu maisha yake sasa na baadaye bila kuwa tegemezi kwa watu wengine kama kupe.
Stadi za afya: mfano wa stadi za afya ni kama vile kuchemsha maji ya kunywa, usafi wa mazingira, usafi wa mwili, matumizi salama ya choo nk. Stadi za afya ni za msingi sana kwa afya ya msichana maana afya ya msichana na jamii yake hutegemea sana stadi hii.
Stadi za ukakamavu: mfano kufanya mazoezi. Ukakamavu ni sehemu ya muhimu ya afya na urembo wa msichana.
Stadi za mawasiliano: mawasiliano ni mchakato wa kutuma na kupokea habari kupitia njia za mawasiliano. Afya ya mwili na akili hutegemea sana jinsi tunavyowasiliana. Stadi hii inahusiana na jinsi msichana anavyoweza kufikisha hisia zake kwa wengine kwa usalama na mafanikio. Inahusisha kuwa na usikivu, uelewa wa ujumbe na namna ya kutumia ujumbe kwa njia inayodumisha afya ya msichana na watu anaokutana nao katika maisha ya kila siku.
Stadi za kuhimili mihemko: sisi ni viumbe tunao kutana na mambo mengi yanayogusa hisia zetu. Mihemko kama vile hasira, aibu, matamanio au woga inahitaji stadi za kuihimili vema na kuidhibiti, vinginevyo mihemko hufanya mtu awe na tabia zinazo dhuru afya yake na afya ya jamii.
Stadi za majadiliano: Msichana anahitaji stadi hii ili kudumisha mahusiano bora na endelevu. Stadi hii inasaidia kudumisha umoja katika kutofautiana. Majadiliano huwezesha kupatikana kwa muafaka bila kuathiri msimamo wa mambo ambayo mtu anayathamini maishani.
Stadi za kufanya maamuzi: stadi hii huwasaidia wasichana kufanya maamuzi mazuri na kutatua matatizo kwa njia bora inayozingatia usalama, ustawi na mafanikio ya msichana mwenyewe na watu wengine ikiwa ni pamoja na kuzingatia matakwa ya sheria na maadili.
Stadi za kuhimili misongo: maisha ya msichana yanakabiliwa na misongo kila kona. Usalama wa msichana na afya ya mwili na akili yake, hutegemea sana jinsi msichana anavyokabiliana na misongo hiyo. Misongo ya masomo, matokeo mabaya ya mitihani, matatizo ya kifamilia, kufiwa na wazazi, umaskini katika familia, kuvunjika kwa urafiki na mambo mengine mengi huleta msongo wa kihisia kwa wasichana wengi.
Wasichana pia hupata msongo kutokana na sura zao au maumbile ya miili yao wanapohisi kuwa hayana mvuto. Yapo mambo ambayo huwezi kuyazuia, mfano mvua ikiamua kunyesha, iache inyeshe hata kama huitaki, ukijitahidi kuizuia unapoteza muda wako. Halikadharika msichana ashughulike na mambo yale anayoyaweza. Kushughulikia mambo yanayokusonga ilihali huna uwezo nayo ni kuongeza msongo unaodhuru afya bila sababu za lazima.
Stadi za kuishi na watu vizuri: kuheshimu na kuelewa mambo ya wengine ni jambo linalodumisha afya ya msichana.
Stadi za kujiamini na kufikiri sawasawa: msichana mwenye stadi hii ana uwezo wa kusimamia kile anacho amini kuwa ni sahihi. Anaongea kwa upole na kwa uhakika. Anapoongea na watu huwatazama usoni katika macho yao, hainami na kuangalia chini wala kutafuna kucha za vidole mdomoni, anaidhibiti aibu yake na kuepuka mabishano na wale wasiokubali maoni yake,a natambua kuwa anaweza.
Stadi ya kuchambua mambo: msichana mwenye stadi hii si mwepesi wa kukubali kila jambo analosoma au kusikia. Anafanya jitihada za kujua chanzo na sababu ya taarifa anazopokea. Stadi hii humsaidia msichana kutofautisha ukweli na ulaghai. Ulaghai ni tatizo la ulimwenguni pote na wasichana wengi ni walengwa wa ulaghai.Wasichana wengi wanaopata mimba katika umri mdogo na afya zao kuathirika vibaya, ni wahanga wa ulaghai.
Msichana mwenye stadi hii hufanya jitihada kuelewa mitandao na magazeti yanayozingatia maadili ya jamii na lengo la kile anachokisoma kama vile kuelimisha, kuburudisha, kufanya biashara, kupotosha ukweli au udaku. Stadi hii humsaidia msichana kuiona mitego na kujua namna ya kuikwepa. Stadi hii pia hukuza kipaji na ubunifu wa msichana.
Stadi za kuwa na mtandao mzuri wa kijamii: Stadi hii husaidia msichana kuwa na marafiki wazuri. Hupata nafasi na fursa ya kupata msaada na kutegemezwa na watu wa familia. Wakati wa matatizo hupata upendo na kutiwa shime ili afikie malengo na kutiwa moyo pale anapokata tamaa. Mtandao mzuri hujengwa na watu wanaojali mafanikio yako, watu wakweli, wenye kujiheshimu na kuheshimu wengine, wanaosikiliza mawazo ya wengine na wasioshinikiza matakwa yao binafsi kufuatwa.

Changamoto za mahusiano ya kijinsia

Changamoto kubwa katika mahusiano ya kijinsia kati ya msichana na mvulana au mwanaume ni ile nguvu ya asili ya uvutano wa kingono. Msichana mwenye mahusiano na mtu wa jinsia tofauti kama hana stadi za maisha, anakuwa sawa na mtu anayecheza na bunduki iliyojaa risasi. Msichana wa aina hii anakuwa sawa na mtu anayetembea juu ya kamba nyembamba katikati ya mto wenye maji mengi na kina kirefu uliojaa mamba wenye njaa kali.
Kuna hatari nyingi za kiafya zinazotokana na mahusiano ya kijinsia yasiyofaa. Kutokana na mahusiano yasiyofaa, wasichana wengi wamekabiliwa na changamoto nyingi kama vile mimba za utotoni, maambukizo ya Virusi vya UKIMWI, magonjwa ya ngono, ugumba na kutopata watoto hapo baadaye, utoaji wa mimba usiokuwa salama, saratani (kansa) ya mlango wa mji wa mimba, msongo wa mawazo, umaskini, kuachishwa masomo, kutofikia ndoto zao za maisha, kukataliwa na kutengwa na wazazi, pamoja na kukosa heshima katika jamii.
Msichana anayejali hali ya afya yake hana budi kukataa kwa nguvu zake zote vishawishi kwa vitendo na maneno yenye nguvu lakini yanayotamkwa kwa heshima na busara. Maneno ya ukali na matusi yakitamkwa kwa mvulana au mwanaume yanaumiza moyo na kusababisha ugonjwa wa kihisia na wakati mwingine yanaweza kusababisha ugomvi. Msichana kabla hajatamka neno lolote ni vizuri alipime ili lisitokeze madhara kwake na kwa wengine.
Msichana kwa namna yoyote ile, asiruhusu maneno kutoroka mdomoni mwake. Ni vizuri kuelewa kuwa mafanikio yetu yanahusiana kwa karibu sana na maneno yetu. Unaweza kufanikiwa au kushindwa kutokana na maneno yako. Wasichana wengi wenye mazoea ya kutumia lugha chafu, matusi na maneno ya jeuri hupoteza nafasi za kupata wachumba na hatimaye kuwa katika wakati mgumu ambao hatimae huwaweka katika hatari ya kupata athari za kisaikolojia hapo baadaye.

Kukabiliana na udhalilishaji wa kijinsia

Udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia kwa msichana ni dalili kuwa hatari kubwa inamkabili msichana. Msichana anaweza kudhalilishwa kijinsia kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na kulazimishwa afanye tendo la ngono na mtu asiyefahamiana naye, mbakaji, mtu anayehusiana naye au mpenzi wake. Msichana pia anaweza kushikwa shikwa sehemu nyeti za mwili wake kama vile matiti, makalio au sehemu za siri au kuambiwa maneno na kufanyiwa mikonyezo inayolenga au kuashiria vitendo vya ngono.
Vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia kwa wasichana ni ukatili na uvunjaji wa haki za msingi za binadamu. Ili kukabiliana na hali hii msichana lazima aepuke mahusiano hatarishi na wanaume. Aelewe kuwa hakuna mtu mwenye haki ya kumdhalilisha kinyume na matakwa yake.
Ikitokea kwa bahati mbaya msichana amebakwa awe mwepesi kutoa taarifa kwa wazazi, walimu au kituo cha polisi, Msichana asione aibu, hofu wala woga wa kutoa taarifa za udhalilishaji aliofanyiwa kwani yeye hakutenda kosa ila ametendewa kosa.Msichana asioge wala kujisafisha ukeni pale anapobakwa kabla hajatoa taarifa polisi na kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya kitaalamu hospitalini.
Kufanya hivyo hupoteza ushahidi wakati anapoenda kupata matibabu na uchunguzi wa kitabibu ambao ni muhimu kwa ajili ya ushahidi utakao mtia hatiani mbakaji. Ni busara kuonana na daktari mapema kabla ya saa 72 kupita ili kupatiwa huduma za matibabu ya dharura yanayozuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI, kuzuia maambukizi ya magonjwa ya ngono na mimba isiyo takiwa.
Ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia na udhalilishaji unaweza kusababisha athari afya ya mwili na athari za kisaikolojia ambazo baadaye kama hazikutibiwa hutokeza ugonjwa wa akili (Rape Trauma Syndrome). Hivyo basi ni vizuri kuonana na mshauri nasaha ili kupata ushauri wa kitaalamu unaosaidia kukabiliana na tatizo hili kwa mtazamo chanya. Lakini pia pale inapowezekana kulingana na imani ya kidini ya msichana, ni vizuri kupata ushauri wa kiroho.

Tohara ya wasichana

Wasichana wanaojitambua wanaelewa hatari za ukeketaji kwa afya ya mwili, roho na akili zao. Ukeketaji ni kitendo cha makusudi cha kukata na kuondoa baadhi ya sehemu za nje za uke wa msichana au mwanamke. Wakati mwingine ukeketaji unahusisha kutoboa na kuziba kwa kushona tundu la njia ya uzazi ili msichana asiweze kuingiliwa na mwanaume yeyote kwa njia ya kujamiiana kabla ya ndoa.
Ukeketaji mara nyingi hufanyika kwa watoto wa kike kati ya umri wa chini ya mwaka mmoja hadi miaka 15. Wasichana wengi hupatwa na madhira haya kutokana na sababu za kimila, kidini na kijamii. Jamii za watu wanaodumisha desturi hii huwa na imani potofu iliyopitwa na wakati na wana itikadi kuwa ukeketaji husaidia kutunza bikira ya msichana na kumfanya awe mwaminifu kabla na baada ya kuolewa. Wanaamini kuwa ukeketaji hupunguza hamu ya tendo la ndoa kwa mwanamke na kwa sababu hiyo wanadhani kuwa ni rahisi kwa mwanamke kutosheka na ngono ndani ya ndoa.
Ukeketaji ni udhalilishaji wa kijinsia na pia ni ukiukaji wa haki za binadamu. Ni kitendo cha unyanyasaji na ukatili. Wakeketaji mara nyingi hukata na kuondoa kabisa kinembe au sehemu ya kinembe au ngozi inayofunika kinembe. Wakati mwingine ukeketaji huusisha kukata na kuondoa midomo midogo ya ndani ya uke na kusababisha maumivu makali kwa msichana.
Msichana aliyekeketwa hukabiliwa na hatari nyingi za kiafya ikiwa ni pamoja na :-
β€’ Kuumizwa kwa misuli ya uke na kusababisha ishindwe kufanya kazi zake kama kawaida kulingana na maumbile ya asili.
β€’ Kumsababishia msichana maumivu makali yanayotokana na kukatwa mwili bila dawa ya kuzuia maumivu (ganzi).
β€’ Kutokwa kwa damu nyingi ambako mara nyingi husababisha hali ya kuzimia na kupoteza maisha wakati mwingine kutokana na upungufu mkubwa wa damu.
β€’ Kupata uambukizo wa magonjwa hatari kama pepopunda (Tetanus), Virusi vya UKIMWI au kuoza kwa jeraha la ukeketaji (sepsis).
β€’ Kuvimba na kuziba kwa njia ya mkojo na kusababisha kushindwa kupitisha mkojo.
β€’ Kupata magonjwa katika njia ya mkojo yatokanayo na uambukizo.
β€’ Makovu ya njia ya uzazi yanayosababisha mwanamke kushindwa kujifungua kwa urahisi kupitia njia ya kawaida. Hii pia huchangia hatari ya vifo vya mama na watoto wakati wa kujifungua.
β€’ Kuharibika kwa afya ya ujinsia ya msichana pindi atakapo olewa. Mara nyingi ukeketaji husababisha hali ya kutofurahia tendo la unyumba na maumivu ya kihisia.
β€’ Msichana imempasa kutambua kuwa mwili wake ni wake na hakuna mtu aliye na haki ya kuchezea mwili huo bila ridhaa yake. Ridhaa hiyo pia lazima ilinde heshima na utu wa msichana, idumishe afya ya mwili, roho na akili.

πŸ™‰πŸ™‰πŸ™‰Usisahau kushare posti hii kuhusu (JINSIA NA MAHUSIANO KWA MSICHANA).πŸ‘ Share facebook, twitter, Google+ n.k bila kusahau WhatsApp! Share kote wenzio nao wasomeπŸ’―βœ”

ml.gif

.