Tafuta

Unatafutwa na marafiki zako wa zamani Bado wanakupenda sana ndio maana wanakutafuta

πŸ‘‰SOMA ZAIDI HAPA...

πŸ‘‰ AFYA NA UREMBO WA MOYONI YA MSICHANAπŸ‘‡βœ”

AFYA NA UREMBO WA MOYONI

Tarakilishi (computer) ni chombo chenye uwezo mkubwa sana wa kufanya kazi nyingi kwa kasi na ufanisi mkubwa. Chombo hiki kimegawanyika katika sehemu kuu mbili; sehemu ya kwanza ni ile ya nje inayoonekana na kushikika (hardware) na sehemu nyingine ni ile ya ndani inayoonekana lakini haishikiki, kwa maneno mengine sehemu hii hujulikana kama program za tarakilishi (software).
Pamoja na umuhimu na uzuri wa umbo la nje la tarakilishi unaomvutia mnunuzi, ukweli ni kwamba bila program za ndani, chombo hiki hakiwezi kufanya kazi yoyote ya maana.
Wabunifu na wasanifu wa tarakilishi wakati wanaanza kubuni na kutengeneza chombo hiki hapo mwanzo, waliiga maumbile na utendaji wa mwili na akili ya binadamu vinavyofanya kazi kimfumo.
Binadamu pia kama ilivyo tarakilishi, tuna sehemu kuu mbili za kimaumbile. Tuna utu wa nje unaoonekana na kushikika pamoja na utu wa ndani moyoni (akilini) unaoonekana kwa matendo na maneno lakini haushikiki.
Wasichana kama walivyo watu wengine wengi, mara nyingi wamekuwa wakishughulikia ustawi, afya na urembo wa utu wa nje unaoonekana na kusahau utu wa ndani. Vyakula, mavazi, mapambo, vipodozi na mambo mengine mengi yamekuwa yakitafutwa kwa bidii sana ili kuhudumia utu wa nje. Mafanikio, ustawi, afya, uzuri na urembo wa utu wa ndani ambao kimsingi ni wa muhimu sana, havipewi kipaumbele kabisa.
Katika jamii yetu leo, urembo wa sura na uzuri wa maumbile huonwa kwa namna tofauti kabisa na zamani. Siku hizi watu wengi hasa wasichana na wanawake wanafikiri kwamba mafanikio ya mtu hutegemea urembo wa sura yake na uzuri wa maumbile ya mwili. Kigezo na mtaji mkubwa wa mafanikio, kupata ajira, nafasi za uongozi, mafanikio ya kiuchumi na mafanikio ya kielimu kwa wasichana na wanawake wengi wa kizazi hiki, hudhaniwa kuwa ni uzuri wa mwili na urembo wa sura.
Kutokana na mtazamo huo, biashara ya bidhaa za urembo, vipodozi, nywele bandia, kucha za bandia, rangi za midomo na nywele, mitindo mipya ya mavazi kila kukicha, matangazo yanayohusu uzuri wa sura na umbo la mwili pamoja na mashindano ya urembo, vimekuwa vitu vyenye kupewa kipaumbele sana hasa miongoni mwa wasichana.
Wasichana wasiotumia vitu hivi vya urembo na mapambo kwa ajili ya miili yao, huonekana ni washamba na wasiokwenda na wakati.Waigizaji wa sinema, wanamuziki maarufu, waandaaji wa vipindi vya runinga (Televisheni), tovuti, mitandao ya kijamii na majarida ya urembo pamoja na magazeti ya udaku, kwa kutumia tekinolojia ya kisasa, wamefanikiwa kukuza (kupromoti) urembo wa sura na umbo na kuwafanya vijana wafikirie kuwa hiyo ndiyo hali halisi na bora zaidi ya maisha na kuwa ndiyo njia ya kufikia mafanikio na furaha hapa duniani.
Katika utafiti mmoja uliofanya na watafiti katika vyuo vikuu vya Regensburg na Rostock (Ujerumani) kuhusu maswala ya urembo, iligundulika kuwa picha nyingi za warembo zinazoonyeshwa katika matangazo mbalimbali ya urembo duniani kote, siyo picha halisi na asilia za warembo bali ni picha zilizorekebishwa kwa tarakilishi(kompyuta) ili zivutie watazamaji kwa lengo la kuwashawishi kibiashara.
Watafiti hawa wanaendelea kusema kuwa watu wengi huwa wahanga wa ulaghai huu na kuchukia sura zao za asili na za wenzi wao kwa kutamani urembo wa kughushi na wa kufikirika tu. Kwa sababu hiyo wengi huwa na ndoto na mahangaiko ya kusaka urembo usiokuwa halisi tena kwa gharama kubwa [24]. Gharama hii inaweza kuwa ya muda, fedha au maisha yenyewe, lakini watu hawajali hayo yote cha muhimu kwao ni kuwa na mvuto wa muonekano.
Vijana wengi hasa wasichana, wameshindwa kabisa kutumia stadi za maisha ya uchambuzi wa mambo na kwa sababu hiyo wameshindwa kuelewa kuwa hiyo ni mitego iliyosukwa na kutegwa kwa ujanja na ustadi wa hali ya juu, ili kuwanasa watu na kuwafanya vitega-uchumi katika mfumo wa utandawazi wa kibepari. Waandaaji wa mitego hii ni watu wanaotafuta kujipatia utajiri bila kujali hasara kwa wateja wao. [25]
Ni jambo la busara kukumbuka kuwa, mafanikio ya maisha na afya ya mwili hayawezi kutenganishwa na mafanikio ya roho zetu pia [26]. Kwa sababu hiyo, mtu mwenye hekima nyingi zaidi aliyepata kuishi katika Israeli ya kale, anakupatia ushauri ufuatao: β€œMwanangu, sikiliza maneno yangu, tega sikio lako uzisikie kauli zangu, zisiondoke machoni pako; uzihifadhi ndani ya moyo wako, maana ni uhai kwa wale wazipatao, na afya ya mwili wao wote, linda moyo wako kuliko yote ulindayo, maana ndiko zitokako chemichemi za uzima.” [27]
Wanawake na wasichana wa zamani waliostahiki heshima, wazuri wa maumbo na warembo wa sura walizingatia mwongozo huu wa kimaadili nao uliwahifadhi dhidi ya hatari na uliwasaidia kupata mafanikio makubwa katika afya na urembo wao wa utu wa nje na utu wa ndani.
Wasichana hao walifanikiwa kuhifadhi ubikira wao (usafi wa kimaadili) wa mwili na roho na kuwaletea heshima na sifa kubwa wao na familia zao. Wasichana hao waliishi katika jamii ya wanaume wenye tabia kama za wanaume wa leo, na wanawake makahaba kama ilivyo leo, lakini hilo halikuwa kikwazo kwa ajili ya mafanikio yao.
Wasichana kama vile Sara, Rebeka, Raheli, Ruthu, Esta, Bikira Mariamu kwa kutaja wachache tunaosoma habari zao katika vitabu vitukufu, ni mifano hai ya wanawake waliofanikiwa kutokana na mashauri haya.
Muumba wa Mbingu na ardhi, aliye tuumba mimi na wewe kwa sura na umbo la kupendeza, anathamini sana uzuri, afya, urembo na mapambo ya utu wa ndani. Moyoni (rohoni) kukiwa na afya, ni rahisi mwili pia kuwa na afya na usalama. Moyo ndiyo taa ya mwili, moyo ukipambwa kwa mapambo mazuri, ni rahisi mwili kupendeza kwani mwili ni mtekelezaji wa maagizo yatokayo moyoni. Ili kutatua matatizo yetu ya nje ni vizuri tukaanza na matatizo ya ndani, tushughulikie chanzo kabla ya kushughulikia matokeo ya matatizo.
Kumbuka kuwa unapojiangalia kwenye kioo na kufikia hitimisho kuwa wewe ni mbaya au sura yako haipendezi au haivutii na kwa sababu hiyo unahitaji ukarabati bandia, tatizo siyo kile unachokiona katika kioo bali tatizo liko katika akili iliyokupatia tafsiri hiyo.
Akili iliyozoezwa kuangalia picha za urembo wa kughushi za wafanya biashara na kusikiliza mapromota wa urembo wa sura na uzuri wa umbo, ni rahisi kutoa maamuzi kwa kutegemea vivutio vya kibiashara.
Mwandishi maarufu aliyeandika vitabu vingi miongoni mwa waandishi mashuhuri duniani aliwahi kusema kwamba, wale wanaotumia muda wao mwingi kuangalia sura zao kwenye kioo, wana mwelekeo mdogo sana wa kuziangalia amri za Mungu kama kioo kikuu cha maadili ya binadamu. [28]
Akizungumza juu ya umuhimu wa afya na mapambo ya moyoni, Mwenye hekima, mfalme wa Israel ya kale, Mheshimiwa Suleimani Daudi, alisema kwamba mwanamke mzuri wa sura asiyekuwa na mapambo ya moyoni (akili), anafanana na pete ya dhahabu iliyowekwa kwenye pua ya nguruwe. [29] Hebu tumia muda wako kidogo kutafakari maneno haya ya mtu mwenye hekima nyingi, piga picha uone pete ya dhahabu iliyonunuliwa kwa thamani kubwa ikigalagazwa na nguruwe kwenye uchafu, matope na uvundo unaonuka, je itaonyesha thamani yake? Eti msichana au mwanamke mrembo asiyetumia vizuri akili yake anafananishwa na pete ya dhahabu iliyowekwa kwenye pua ya β€˜kitimoto’.
Mtu maarufu sana kuliko wote waliopata na watakaopata kuishi duniani, Yesu Kristo (Masihi Issa bin Mariam) naye aliwahi kuzungumza na kutoa msisitizo kuhusu uzuri wa ndani ya moyo wa mwanadamu. Yeye alisema kuwa uzuri wa nje bila uzuri wa ndani ni sawa na kaburi lililopakwa rangi nzuri kwa nje lakini ndani yake kuna mifupa ya wafu na uchafu (uozo) wote. [30]
Mwandishi mwingine maarufu wa karne ya kwanza aliwahi kuandika kuhusu urembo na mapambo yenye maana zaidi kwa wanawake na wasichana, naye alisema, β€œKujipamba kwenu kusiwe kwa nje …, bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika, yaani, roho ya upole na utulivu iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu, maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani…”.[31]
Mfalme, mwandishi na mtunzi mashuhuri wa mashairi mnamo miaka ya 400 kabla ya Kristo, naye aliandika juu ya umuhimu wa mapambo ya moyoni akisema kuwa BWANA huwapamba wenye upole kwa ajili ya wokovu. [32]
Kiongozi mmoja maarufu wa mambo ya kidini na afya ya kiroho naye aliandika juu ya mapambo na urembo kati ya mwaka 647 na 580 kabla ya Kristo (K.K) akasisitiza kuhusu umuhimu wa mapambo ya moyoni. Kuhusu mapambo ya utu wa nje yeye alikuwa na haya ya kusema, β€œUjapojitia mavazi mekundu, ujapojipamba mapambo ya dhahabu, ujapojitia wanja machoni, unajifanya kuwa mzuri bure tu; wapenzi wako wanakudharau, wanakutafuta roho yako (ili wakuangamize). [33]
Isaya Amozi, kiongozi wa kidini aliyepata kuishi katika jiji la Jerusalemu nchini Israel, naye aliwahi kuandika juu ya wale wanaothamini sana afya na urembo wa mwili na kudharau afya na urembo wa moyoni. Isaya alisema kuwa siku moja MUUMBAJI atawaondolea watu hao mapambo ya pete za masikio (hereni),vikuku, azama (vishaufu au vipini vya puani), vibweta vya marashi, shali(mtandio wa kujitanda mabegani), vifuko(vipochi), vioo vidogo (kwa ajili ya kujiangali usoni mara kwa mara), mavazi ya sikukuu(mavazi ya gharama kubwa sana) na vilemba vyao. Hata itakuwa badala ya manukato mazuri kutakuwa na uvundo, badala ya mishipi (mikanda), watavaa kamba; na badala ya nywele zilizosukwa vizuri watakuwa na upara; na badala ya kisibao (kitop), watavaa mavazi ya kigunia; na kutiwa alama mwilini kwa moto badala ya uzuri (mapambo ya kujichora) [34]
Hadithi nyingi zilizosimuliwa na maswahaba wa Mtume Mohammad (S.A.W) pia zinaonyesha kuwa Mohammad (Rehema na amani ziwe juu yake), alitahadharisha sana kuhusu athari za kujipamba kwa nje na kusahau umuhimu wa kujipamba kwa mapambo ya moyoni. Alikemea juu ya kujipamba kupita kiasi, kujichora kwa tattoo mwilini pamoja na kujibadilisha rangi ya ngozi. Moja ya hadithi muhimu katika jambo hili ni ile inayopatikana katika Ibn Majah Vol. 3, Juzuu ya 9, Hadith 1987.
Daktari mmoja kutokana na uzoefu wake wa siku nyingi katika maswala ya vyanzo vya magonjwa ya binadamu, pia anailinganisha hali ya kupuuza ushauri na mwongozo wa neno la Muumbaji wetu, kutokumtegemea Mungu pamoja na kutokufanya ibada, sawa na vyanzo vingine vya magonjwa kama vile matumizi ya dawa za kulevya (tumbaku na ulevi wa pombe). [35]
Ukweli ni kwamba, afya ya kiroho na mapambo mazuri ya moyoni vinapokosekana, moyo (akili) ya mtu huingiliwa na sumu zitokanazo na hisia mbaya zisizodhibitiwa na kanuni za maadili. Hofu, woga, wasiwasi, hasira, kujichukia, ghadhabu, hamaki, sonona na msongo mkali wa mawazo, hutokeza madhara kwa afya ya mwili, akili na roho.
Ni jambo la busara kuelewa kuwa thamani ya msichana au mwanamke, haitokani na mapambo, vipodozi, urembo wa uso au uzuri wa umbo, bali hutokana na maadili mema na sifa njema zinazoupamba utu wake wa moyoni. Akifafanua jambo hili, mwenye hekima aliandika akisema, β€œUzuri ni ubatili; bali mwanamke amchaye BWANA, ndiye atakayesifiwa. [36] Hii ni kwa sababu β€œBWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo”. [37]
Wasichana wanaomcha BWANA, wasiosahau sheria yake na wanaozishika kanuni za afya zilizoko ndani ya amri zake, huongezewa wingi wa siku na miaka ya uzima na amani, nao hupata afya njema ya mwili na mifupa yao hulainishwa kwa mafuta.[38] BWANA huwaondolea maradhi na kuwaponya magonjwa yao.[39] Moyo wao huchangamka na hii huwa dawa nzuri na ya uhakika kwa afya ya miili, akili na roho zao. [40]

Msichana na viwango vya ubora wa mwanamke

Hakuna mwanamke ambaye hajawahi kupitia katika hatua ya usichana, hii inamaanisha kuwa wanawake na akina mama bora hapa duniani wanatokana na wasichana bora. Usichana ndiyo maabara ya kuzalishia wanawake bora, kama jamii au taifa litakuwa na wasichana wenye viwango duni vya elimu, maadili, fikra, afya na urembo, basi hatutegemei kuwa na akina mama bora katika siku za usoni. Hatutegemei kuwa na wake za watu wanaojua kutunza ndoa zao na kulea familia.
Katika mfumo wa maisha ya kisasa ambapo utandawazi, biashara na soko hulia vinatazamwa kama mtindo unaoharakisha maendeleo ya binadamu, tunakabiliwa na tatizo la bidhaa zisizokuwa na viwango vya ubora. Akili za watu zinaanza kuzoea kuona viwango duni kama sehemu ya maisha ya kawaida. Hali hii ya kushuka kwa ubora wa viwango haiishii katika bidhaa peke yake, lakini pia inaathiri viwango vya ubora wa maisha, afya na tabia za watoto, wavulana, wanaume, wanawake na wasichana.
Mheshimiwa Daudi, Mfalme wa Israel ya kale na mwandishi wa Zaburi, alipozungumza kuhusu viwango vya ubora wa vijana na urembo halisi wa wasichana alisema maneno yafuatayo: β€œWana wetu wawe kama miche waliokua ujanani, na Binti zetu kama nguzo pembeni zilizonakshiwa na kupamba hekalu…”[41]
Bila shaka wasichana wanaolelewa katika maadili ya kumcha na kumheshimu Mungu na kuendelea kuheshimu viwango vya hali ya juu vya maadili, hawa huwa ni mbaraka mkubwa katika jamii yao. Katika kipindi hiki, wazazi wengi kutokana na shughuli za kimaisha hawapati muda wa kutosha kuhakikisha kuwa wasichana wao wanafundishwa mambo muhimu yatakayowafanya kuwa wanawake wenye viwango bora hapo baadaye.
Kuwa mzazi ni jukumu zito, kuliko wengi tunavyofikiri. Akina mama wanayo majukumu ya ziada kuhakikisha kuwa wasichana wanapewa uangalizi na matunzo bora yatakayowafanya wawe na afya njema ya kimwili, kiakili na kiroho. Hatuwezi kuacha jukumu la malezi kwa watoto wetu wa kike, na kuwaacha wajilee wenyewe hata kama tunahisi kuwa wamekuwa wakubwa na wanasoma katika shule za sekondari au vyuo vya elimu ya juu.
Katika kipindi hiki wasichana huwa katika wakati mgumu sana wa mabadiliko ya makuzi na wakiachwa wajichagulie mambo ya kufanya bila mwongozo mzuri wengi hupoteza mwelekeo. Mawazo ya wasichana katika kipindi hiki cha makuzi, yanatembea huku na kule wakati wote na yanaathiriwa vibaya sana na mambo yasiyofaa kuliko kipindi kingine chochote katika maisha yao.
Wasichana wengi wanaathiriwa na mtindo wa maisha wa kimagharibi, wanaiga maisha ya wasichana wenye maadili mabaya wa Ulaya na Marekani wanaoonyeshwa katika vyombo vya habari na filamu. Wengi hutamani kwenda kuishi huko na wengine hupelekwa na wazazi huko kwa ajili ya masomo. Lakini wengi wanashindwa kumaliza masomo yao kutokana na kujiingiza katika magenge ya wasichana wenye tabia na mienendo isiyofaa na wengi hupoteza mwelekeo na kuacha maadili mema. Wengine hujiingiza katika biashara haramu ya ngono, dawa za kulevya na utengenezaji wa filamu za ponografia.
Wengine pia hujiingiza katika ndoa za ajabuajabu ili kupata vibari vya kufanya kazi katika nchi hizo. Wengine huwa katika mapambano na mapigano na wenyeji wa nchi hizo, jambo ambalo huwaacha wengi wao wakawa hoi kwa michoko ya kimaisha.
Elimu na mtindo wa maisha wa nchi za Magharibi vimegeuka kuwa miungu fulani katika kipindi hiki cha siku zetu. Maisha ya kumcha Mungu na kuheshimu maadili mema, yamepoteza mvuto kwa wasichana wengi na yamekuwa sawa na mpando ulioinuka kuelekea mlimani. Simaanishi kuwa mtindo wa maisha katika nchi za Magharibi ni mbaya kwa ujumla, ila mila zao kwa kiasi kikubwa sasa hivi zinakinzana na maadili mema.
Ili wasichana wa leo wafae kuwa wanawake bora, wanahitaji mafunzo (training), kwani siku za usoni tunawatazamia wao kuwa walimu wa watoto wao na watahitaji kuwa na mawasiliano bora na waume zao pamoja na wakwe. Wasichana wa leo ndio wanaotazamiwa kuwa waalimu wa awali wa viongozi wa mataifa ya siku za baadaye.
Ni busara wasichana wajue jinsi ya kuepuka makosa yasiyokuwa ya lazima na wajue jinsi ya kuomba na kutoa msamaha, kwani hakuna ndoa inayoweza kudumu bila kujali msamaha. Wasichana inawapasa kujizoeza tabia ya uaminifu na uadilifu itakayokuwa msingi wa ndoa katika siku za usoni.
Wasichana wajizoeze kuwa wasikivu bila kuingilia kati katika mazungumzo, kubishana au kupayuka payuka. Hii itasaidia kupunguza idadi ya taraka na kuvunjika kwa ndoa nyingi kunakosababisha mateso kwa mamilioni ya watoto wasiokuwa na hatia.
Katika kitabu cha Mithali sura ya 31 mfalme Suleimani Daudi wa Israel ya kale anatujuza mambo mengi ya msingi yanayoweza kumfanya msichana kuwa mwanamke bora. Suleimani anamzungumzia mwanamke huyu kwa undani sana.
Twaona kuwa mwanamke bora anahakikisha famila yake inapata chakula cha kutosha, mavazi na mahitaji mengine muhimu, anafanya ujasiriamali, ananunua mashamba na kufanya kilimo cha mazao ya chakula na biashara, ananunua nyumba na anasaidia wenye mahitaji. Ni mwanamke wakupendeka (admired) anayejua kujipamba kwa mapambo ya mwilini na moyoni. Wanaume wengi wangependa kuwa na mke mwenye sifa hizi, akina kaka wengi wangependa kuwa na dada mwenye sifa hizi na watoto wengi wangependa kuwa na mama mwenye sifa hizi.
Ili msichana afikie viwango vya ubora anavyovitaja mfalme Suleimani ni lazima alelewe na kufundishwa tangu anapokuwa mdogo hadi katika kipindi cha kuwa mwanamke. Ajue wajibu wake kama msichana na hapo baadaye atakapo kuwa mwanamke, ajue jinsi ya kupanga mipango ya maisha yake na familia yake na aelewe jinsi ya kutumia rasilimali na fursa anazopata kwa faida yake na familia kwa ujumla.
Ni vizuri kutambua kuwa ubora wa familia huanzia kwa mwanafamilia mmojammoja, ubora wa jamii huanza na ubora wa familia na ubora wa taifa huanza na ubora wa jamii. Wote tungependa tuwe na mabinti waliokomaa kiroho, kiakili, kijamii, kiuchumi na kimwili pia kwa ajili ya mstakabari mwema wa jamii.
Wasichana lazima wajifunze kupangilia mambo, wajue kupanga nyumba vizuri ili kuleta mawazo yaliyotulia na kuakisi tabia ya Mungu ambaye ni muasisi wa mipango na uzuri (beauty). Wasichana wafanye ziara za mafunzo katika nyumba za wanawake waliopanga vitu vizuri na kwa idhini yao wajifunze jinsi wanavyopanga jiko, makabati au sebule zao.
Wajifunze jinsi ya kutunza kumbukumbu muhimu za nyumbani kama vile kadi na vyeti vya hospitali, kadi za maendeleo na chanjo za watoto, masanduku ya huduma ya kwanza, faili au daftari lenye namba za simu muhimu za watu na huduma kama vile jeshi la zima moto, namba za polisi, namba za dereva wa taxi wakati wa dharura, risiti za kununulia vitu, marakaratasi ya bima, vitambulisho na mambo mengine muhimu.
Wasichana wajifunze kupanga na kuweka picha vizuri ukutani na katika album za picha. Wajizoeze kuweka kila kitu mahali kinapotakiwa kuwa, hata akivua nguo zake usiku wakati wa kulala, asizitupe hovyo sakafuni bila kuzikunja na kuziweka kwa utaratibu hata kama ni chafu.
Msichana asizoee kurundika vitu badala ya kupanga; kabati la nguo, pochi, begi la shule, viatu na vitu vingine lazima vipangiliwe vizuri. Ajifunze kupangilia na kutunza muda na kuepuka tabia ya kuchelewa mahali anapotakiwa kuwa na ajizoeze kumaliza kazi kwa wakati uliopangwa. Ajue vitu vyake vilipo na asitumie muda mwingi kuhangaika kutafuta vitu vyake bila mafanikio. Lakini zaidi msichana lazima ajue kuandaa chakula kizuri na chenye viini lishe vinavyodumisha afya na uzuri wa mwili.
Wageni tunaowaalika majumbani mwetu watapenda kuona kama nyumba zetu zina utulivu na mipangilio mizuri. Binti aliyejifunza kupanga vitu na kupamba nyumba akiwa mdogo atakuwa msaada kwenye familia yake na hata kazini kwake. Atasaidia katika jukumu la kudumisha usalama na afya ya mwili na akili katika jamii na mahala pa kazi. Vitu ambavyo havikupangiliwa vizuri ni rahisi kusababisha ajali na wakati mwingine husababisha akili kukosa utulivu na kupunguza ufanisi wa kazi.
Wanawake wengine wanazaliwa na talanta ya kupanga na kupamba vitu vizuri, mfano mzuri ni wanawake wa mashariki ya mbali wanaopangilia maua vizuri sana, na wasichana wengi wanahitaji kujifunza na kuhimizwa tena na tena kuhusu usafi na mipangilio mizuri ya nyumba wanazokaa na wajifunze kutandika vitanda vyao kila siku wanapoamka asubuhi ili kuwa na mwonekano nadhifu.
Mwanazuoni Paulo katika kitabu cha 1Wakorintho 14:40, anaripoti kuwa mpangilio mzuri ni moja ya sheria muhimu za maadili. Ni kanuni ya maisha kuwa vitu vikubwa hutengenezwa na vitu vidogovidogo, ukijizoeza kutekeleza majukumu madogomadogo kwa ufanisi, tabia hiyo itakusaidia kujenga mazoea ya kutimiza majukumu makubwa kwa ufanisi mkubwa pia.Ukiwa mwaminifu kwa mambo madogomadogo uatajijengea msingi wa kuwa mwaminifu katika mambo makubwa pia.
Wewe unayesoma kitabu hiki sasa, hebu tumia mashauri haya ambayo Muumba wako ameona vema kuruhusu yafike kwako kwa wakati muafaka na kwa kusudi maalumu, ili yakusaidie kufanya mabadiliko chanya yatakayokuletea manufaa na mafanikio ya kimwili, kiakili na kiroho, wewe, familia yako, jamii yako, taifa lako na jumuia ya kimataifa.
Tumia mashauri haya kwa ajili ya kujitayarisha kwa ajili ya ubora wa maisha yako ya sasa yaliyobaki. Tumia mashauri haya pia kwa ajili ya maandalizi ya kuwa na ndoa na familia yenye furaha na mafanikio. Tumia mashauri haya pia kwa ajili ya maandalizi ya kupata maisha bora yaliyoko ng’ambo ya kaburi wakati ambapo wenye afya ya kiroho na urembo wa moyoni, watakapo rejeshewa afya na urembo wao wa asili uliopotezwa na wazazi wetu wa awali. Wakati ambapo watu hawatahitaji sindano ili kuwa na afya wala makopo ya vipodozi ili kuwa warembo.
Ni ombi langu kwa ajili ya msichana au mwanamke yeyote aliyebahatika kusoma kitabu hiki kuwa, maarifa haya yawe kama buruji (boma la ngome) za madini ya fedha na kama mbao za mierezi katika kukuhifadhi salama kiafya. Nami naungana na vijana wenye busara wanaopatikana katika kitabu cha kale zaidi cha afya ya jamii, maadili na mwongozo wa maisha bora, waliomjali na kumlinda mdogo wao wa kike (msichana) ili apate mafanikio katika maisha hata wakasema maneno yafuatayo:
β€œKwetu sisi tuna umbu mdogo,
Wala hana maziwa;
Tumfanyieje umbu letu, siku atakapoposwa?
Kama akiwa ukuta (imara),
Tumjengee buruji za fedha;
Na kama akiwa ni mlango (dhaifu),
Tumhifadhi kwa mbao za mierezi” [42]
Nawe mara upatapo maarifa haya, yatumie kulinda afya na urembo wako ili ujipatie amani ya moyo na uungane na msichina huyu kwa kushukuru na kusema:
β€œMimi nalikuwa ukuta,
Na maziwa yangu kama minara;
Ndipo nikawa machoni pake,
kama mtu aliyeipata amani”. [43].

πŸ™‰πŸ™‰πŸ™‰Usisahau kushare posti hii kuhusu (AFYA NA UREMBO WA MOYONI YA MSICHANA).πŸ‘ Share facebook, twitter, Google+ n.k bila kusahau WhatsApp! Share kote wenzio nao wasomeπŸ’―βœ”

Marafiki zako wa zamani utawakuta hapa sasa Bado wanakupenda sana na wanakungoja kwa hamu kubwa

πŸ‘‰SOMA ZAIDI HAPA...

Marafiki-wa-enzi.GIF

.