Iwapo msichana atajamiiana wakati wa siku salama anaweza kuepuka kupata mimba?

Siku salama ni siku ambazo hakuna yai ambalo lipo tayari kwa kurutubishwa. Iwapo mwanamke atajamii ana katika siku salama tu, yaani wakati ambapo hakuna yai lililo tayari kurutubishwa, anaweza asipate mimba. Hata hivyo, i inatakiwa ajue kwa uhakika lini yai linakuwa tayari kurutubishwa.
Kwa vile wasichana wengi mzunguko wa siku zao hubadilika kila wakati, ni vigumu kujua kama kuna yai ambalo lipo tayari kwa kurutubishwa. Mzunguko na siku za hedhi za msichana unaweza kuathirika na mfadhaiko, huzuni, maradhi, safari au mabadiliko mengine katika maisha ya msichana. Hata kama msichana atakuwa na mzunguko ambao haubadilikibadiliki anaweza kupata mabadiliko ya ghafla katika kipindi fulani.
Kwa hiyo, kuhesabu siku salama siyo njia salama ya kuepuka kupata mimba. Kwa upande wa wasichana hakuna siku salama kutopata mimba, kwa sababu mzunguko wa siku zao za hedhi unabadilika badilika hata zaidi kuliko ule wa wanawake watu wazima!