Mtu aliyefanya kazi ngumu zaidi afunguka

By, Melkisedeck Shine.

elimu-sayansi-na-tekinolojia.png

Mtu aliyefanya kazi ngumu zaidi afunguka

*SIMULIZI YA KUSISIMUA*
👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾👇🏾🤔
*Mtu aliyefanya kazi ngumu zaidi afunguka*

Wanaopatikana na hatia ya kuua kwa
kukusudia huhukumiwa kifo.

Japokuwa kila
nafsi itaonja mauti, wanaohukumiwa kifo
ndio huweza kujua siku na aina ya kifo.

Hivi mtu akihukumiwa kifo na mahakama, je,
wanaofanya kazi hiyo ni nani? Kitanzi
kikoje? Hali inakuwaje kabla? Je, hupata
fursa ya kuaga ndugu na jamaa?

Wanaotekeleza hukumu ya kunyonga wenzao hadi kufa pia wanakuwa wametenda kosa la kuua, je, huchukuliwa hatua gani kisheria?

Je, wanaoajiriwa kufanya kazi hiyo
wanapatikanaje? Wanajisikiaje kukatisha uhai wa wenzao?

Lakini pia katika utumishi wao, ufanisi wao unapimwaje? Je, hupata utulivu wa moyo na amani kiroho?

Kwa kawaida kazi nyingi hutangazwa wazi magazetini na wale wanaojiona wana sifa zinazohitajika, huandika barua za kuomba na
kusubiri kuitwa kwa mahojiano. Lakini, ni
vigumu kukutana na tangazo la kazi hii
ngumu kuliko zote.

Pia, najua kwamba baadhi ya kazi huhitaji
wasomi wa kiwango cha juu, nyingine watu
wenye ujuzi fulani lakini zipo zinazohitaji
wenye nguvu.

Binafsi nadhani kazi hii inahitaji watu wenye moyo wa ujasiri ambao hawawezi kukosa utulivu wa moyo wala amani kiroho
wakitekeleza jukumu lao kwa watu
waliohukumiwa kifo.

Maswali hayo na mengine mengi nimekuwa
nikijiuliza kwa siku nyingi na katika
kufuatilia nililazimika kufunga safari hadi
mkoani Dodoma ambako nilifanikiwa
kumshawishi mtekelezaji wa hukumu hizo
afanye mahojiano nami.

Saa 12.00 jioni, nikiwa na mwenyeji wangu
wa Dodoma tulifika nyumbani kwa mtu
tuliyekuwa tukimtafuta, Anangisye (siyo jina lake halisi).

Huyu ni askari mstaafu aliyefanya kazi Jeshi
la Magereza kwa miaka 32 huku akitumia
miaka 22 kufanya kazi hiyo maalumu ya
kutekeleza hukumu za kifo.

Tulipokewa na mjukuu wake, ambaye
alituambia kuwa babu yake aliondoka
nyumbani tangu asubuhi. “Shuuuuu,”
tulishusha pumzi ikiwa ni ishara ya kukata
tamaa, lakini kijana yule alitusihi tuvute
subira.

Kijana yule alitukaribisha ndani na wakati
tunaingia mama mwenye nyumba, Matilda (pia siyo jina lake halisi) alitupokea na
kutukaribisha sebuleni.

Tunaingia katika nyumba hii, ya matofali, ina
vyumba vitano na sebule. Vyumba vitatu
vimepangishwa na vingine vinatumiwa na
Anangisye na familia yake.

Mimi na mwenyeji wangu tukaendelea kukaa sebuleni tukimsubiri Anangisye huku mama
mwenye nyumba akituelezea jinsi jino
linavyomsumbua.

Baada ya robo saa hivi, sauti ya mwanamume
ilisikika nje huku mama mwenye nyumba na
yule kijana wakisema, “huyoo”.

Alipokuwa anaingia sebuleni, sote tulisimama
na kusalimiana naye huku tukikumbatiana
kana kwamba tulifahamiana siku nyingi.

Punde alimwita mjukuu wake na kumtuma
dukani akatununulie soda.

“Mnasema mnataka kujua kuhusu kazi
maalumu?” aliuliza Anangisye nami nikajibu,
“ndiyo baba”.
“Mnanitafutia kazi nini maana nimestaafu
tangu mwaka 2006,” alisema katika hali ya
masihara.

Mara alibadilika na kusema kwa utani.
“Lakini endapo itatokea kazi ya kunyonga
niko tayari kufanya kwa sababu hakuna mtu
yeyote anayeiweza kazi hiyo zaidi yangu,”
alisema.

Anangisye ni mcheshi na mkarimu na wajihi
wake ni mrefu, mnene, mwenye sauti nzito
na anayependa masihara.

Baada ya masihara ya hapa na pale,
Anangisye alianza kusimulia historia yake,
alivyosoma, alivyopata kazi na jinsi
alivyokuwa akitekeleza wajibu wake huo bila
hofu.

Huku tukiwa tumetumbua macho na
tukirekodi sawia maelezo yake, Anangisye
alieleza kwa ufasaha kazi hiyo. Na hii ndiyo
simulizi yake:

Mimi bwana ni mzaliwa wa Mbozi, sasa iko
mkoani Songwe. Nilisoma hadi darasa la nane
katika Shule ya Kati wilayani Mbozi.

Mwaka
1974 niliomba kazi ya uaskari magereza.
Nilipopata ajira nilipangwa gereza la
Sengerema, Mwanza.

Huko nilifanya kazi kwa muda mrefu tu
nikiwa askari wa kawaida wa magereza.

Mwaka 1984, yaani baada ya kufanya kazi
kwa miaka 10 lilitolewa tangazo na Wizara ya
Mambo ya Ndani kwamba anahitajika mtu
kwa ajili ya kazi ya maalumu. Niliposikia
tangazo lile bila wasiwasi wowote niliomba.

Basi, baada ya muda nikaitwa na Kamishna
Mkuu wa makao makuu ya Magereza, Dar es
Salaam. Nilipofika Kamishna akaniuliza:
“Wewe ndiye Anangisye?”
“Nikamjibu, “ndiyo”.
Akaniuliza tena kama niliomba kazi maalumu
na nikamjibu “ndiyo”.
“Basi umekubaliwa,” akasema.

Baada ya kuambiwa hayo nilielezwa zaidi
kuwa Jeshi la Magereza limechagua watu
wawili, yaani mimi na mwenzangu mmoja
ambaye niliambiwa tutakutana Gereza la
Isanga, Dodoma ambako kutakuwa kituo
kikuu cha kazi yetu.

Niliambiwa kuwa kuanzia siku hiyo
nitapelekwa Isanga na nitaripoti kwa RPO.
Kwa hiyo nikawa nimeondolewa Sengerema.

Nilipofika Isanga nilitambulishwa kwa
mwenzangu na nikaambiwa kuwa tupo
wawili tu nchi nzima na tutafanya kazi hii
maalumu pale inapotokea na maelekezo
mengine tutaendelea kuyapata.

Tuliambiwa kuwa tutakuwa tunafanya hiyo
kazi nchi nzima, tutakuwa tunazunguka
mikoani pale ambapo kazi zitatokea.

*Kozi ya kunyonga*
Kitu cha kwanza baada ya kukubaliwa kupata
kazi hii mimi na mwenzangu tulipewa
mafunzo maalumu kwa muda wa mwezi
mmoja palepale Isanga, tukafuzu, sisi wawili
tu.

Mafunzo yetu yalihusisha namna ya kufanya
kazi hiyo, namna ya kutumia kamba, mikanda
ya kumshikilia mtu anayenyongwa pamoja na
maandalizi yake.
Kuna namna ya kufunga kile kitanzi, ni
lazima kiwe imara na salama ili yasitokee
makosa. Lakini pia mikanda na eneo lenyewe
na tulielekezwa jinsi ya kumweka mhalifu
katika kitanzi chenyewe.

Katika ufanyaji kazi tulikuwa tunalindwa na
askari magereza. Kwa mfano, siku ya kufanya
kazi, tulikuwa tunasindikizwa na askari
wakati wa kwenda na kurudi. Ilikuwa lazima
tulindwe na ulinzi mkali wa askari ili isije
kutokea tukapata madhara na kushindwa
kutimiza wajibu wetu kwa sababu tulikuwa
sisi wawili tu.

Kwa mfano, tulipotakiwa kufanya kazi Mbeya
tulikuwa tunapewa ulinzi wa askari kutoka
Dodoma hadi Mbeya na tulikuwa tunapewa
huduma za hali ya juu za malazi na chakula
ili tuwe na nguvu.

Kitu kingine ni kwamba ule usiku wa
kuamkia siku ya kazi, tulikuwa tunapewa
pombe. Mimi nilikuwa nakunywa bia aina ya
Safari; basi unawekewa hata kreti zima,
tunakunywa, tunakunywa hadi asubuhi.

Hadi ninapoamka asubuhi bado nakuwa na
pombe kichwani; kabla ya kazi kuanza bado
nakuwa na mning’inio wa pombe kichwani.
Jambo hili lilikuwa linatusaidia sana kufanya
kazi yetu vizuri na kwa ujasiri.

Mwisho wa mwezi tulikuwa tunalipwa
mshahara mzuri tu na pia tulikuwa tunalipwa
posho. Kwa wakati ule, kila tukitekeleza kazi
tulikuwa tunapewa Sh700 kwa kichwa,
baadaye katika miaka ya 1990 posho hii
iliongezeka hadi Sh5,000 na baadaye miaka ya
mwanzoni mwa 2000 tulipewa Sh50,000.

Halafu nilikuwa na ofa ya kutofanya kazi
nyingine yoyote.

*Matanga kabla ya kifo*
Unajua vifo vingine vyote hutokea ghafla,
lakini kifo cha kuhukumiwa kunyongwa hadi
kufa kinajulikana.

Mhalifu anajua kifo chake
tangu siku anaposomewa hukumu yake ila
anachosubiri ni kutekelezwa kwa hukumu
hiyo basi.

Kwa utaratibu wa magereza, mhalifu
aliyehukumiwa kifo, hutayarishiwa matanga
siku moja kabla ya kunyongwa.

Wanamweka
katika chumba maalumu; kila mmoja kwenye
chumba chake.

Wanamfungia humo na
wanampa chakula na huduma yoyote
anayoitaka, hayo ndiyo matanga yake.

Wakati waliohukumiwa kifo wakiwa kwenye
matanga, wafungwa wengine huimba nyimbo
za maombolezo kama sehemu ya kuwaombea
wenzao kabla kifo hakijawameza. Matanga
hayo ni ya siku moja tu.
*Atekeleza hukumu kadhaa*
Nimesema nilianza kazi hii mwaka 1974 na
nilistaafu mwaka 2006. Nimefanya kazi ya
askari magereza kwa miaka 32 lakini pia
nimefanya kazi hii maalumu kwa miaka 22.

Nakumbuka kwamba katika kipindi changu
cha kazi nimewahi kunyonga watu zaidi ya..
(kwa sasa hatutataja idadi).

Kabla ya kumweka kitanzini, mfungwa yeyote
huwa na maandalizi yake. Viongozi wa dini
zote mbili za Kiislamu na Kikristo huitwa,
wanafika magereza na kuwaongoza wahalifu
sala ya toba.
Huo ndio utaratibu.

Wakishafanyiwa sala ya
toba au kuongozwa sala yoyote ile inayofaa
kabla ya kifo, huwekwa tayari kwa ajili ya
kunyongwa.

Anakuwepo pia mwanasheria wa magereza au
korona. Haiwezekani wakanyongwa bila ya
kuwepo viongozi wa dini.

Hanyongwi mtu mmoja, inawezekana kwa
siku moja wakawa watu wanane au kumi,
inategemea na waliohukumiwa mwezi huo.

Baada ya kutekeleza hukumu hiyo kwa mtu
mmoja, nilikuwa naenda kupumzika kwa
dakika 45 kabla ya kuendelea na kazi hiyo
kwa mtu mwingine.

Kwa kawaida kazi huanza saa 2.00 asubuhi,
baada ya kumaliza kazi tunakwenda
kupumzika ofisini, tunakunywa kinywaji
pale, baada ya dakika 45 tunarudi tena
kuendelea na kazi.

Baada ya mapumziko ya dakika 45,
tunakwenda kuangalia kama ameshafariki
dunia, tukimaliza kuhakiki tunaendelea na
wengine hadi waliopangwa siku hiyo
wameisha. Kwa siku walikuwa watu wanane
kutegemeana na idadi ya waliohukumiwa na
kitanzi kinaweza kutumiwa na watu watatu
kwa mpigo. Kwa hiyo, tukimaliza watatu,
tunasubiri na kuendelea na kazi.

*Kitanzi kilivyo*
Kitanzi kilivyo ni kamba iliyoning’inizwa juu
kwenye mbao katika eneo mfano wa chumba
ambalo pia ni kama shimo. Anayenyongwa
husimama juu ya mbao akiwa ameshikiliwa
na kufungwa kitambaa cheusi usoni.

Sisi tunaingiza kitanzi kwenye shingo. Ubao
huwa umeegeshwa na kazi yetu ni kufyatua
kitufe mfano wa gia ya gari, na kikifyatuliwa
humfanya huyo mtu kuning’inia na hapo
kitanzi humkaba.

Sisi kazi yetu ni kufyatua tu kitanzi, baada ya
mtu kuning’inia na kuhakikisha kuwa
amekufa, tunaondoka.

Askari wengine wana
kazi ya kuitoa miili na kuipanga kwenye
vitanda vilivyojengwa kwa sementi ambavyo
vipo katika chumba cha kitanzi.

Baada ya kumaliza kazi yetu, kuna askari
ambao wana kazi ya kuwatoa nje na kuanza
shughuli za kuwazika, kazi ambayo hufanywa
ikihusisha wafungwa wachache na askari tu.

Hii kazi haiwezi kuhusisha ndugu wa
wafungwa, bali kundi dogo la wafungwa
linatengwa kwa ajili ya kuhudhuria mazishi
hayo.

*Mashtaka kortini*
Ingawa kazi hii maalumu hufanywa kwa
mujibu wa sheria, baada ya kumaliza
walikuwa wananipeleka mahakamani na
kunisomea mashtaka kama muuaji mwingine
yeyote. Lakini nilikuwa najibu kuwa mimi
nimeua kwa mujibu wa sheria.

Baadaye utaratibu huo ulibadilishwa baada ya
Serikali kuona kuwa kusomewa mashtaka
mbele ya mahakama huku kukiwa na raia
kunaweza kuhatarisha maisha yetu. Baadaye
wakabadilisha nikawa nasomewa mashtaka
mbele ya mkuu wa magereza tu.

Nikimaliza kusomewa mashtaka na mimi
nilikuwa najitetea kwa kutumia vifungu vya
sheria, basi naachiwa huru na kuendelea na
kazi zangu.

Hapo nikaingilia na kumuuliza: “Ulikuwa
huwaonei huruma?”
Huruma itoke wapi wakati tayari nimeapa na
ninatelekeza kazi yangu kwa mujibu wa
sheria? Wale watu mara nyingi walikuwa
wanalalamika na kutoa maneno makali pale
panapoanza kuwekewa kitanzi.

Wanalalamika
na kusema ‘sisi tunatangulia lakini hata ninyi
mtatufuata tu’ ila sisi hatuzungumzi chochote
tunatekeleza.

*Nataka kazi tena*
Sasa hivi nimestaafu tangu mwaka 2006,
lakini endapo itatokea kazi hiyo niko tayari
kufanya kwa sababu hakuna mtu yeyote
anayeiweza kazi hiyo zaidi yangu. Hapa
Tanzania nipo peke yangu mwenye ujuzi huu,
kwa hiyo ikitokea kazi wakiniita mimi
nafanya tu kwa sababu ni kazi kama
nyingine.

Mwenzangu tuliyeanza kazi pamoja alifariki
mwaka 2002. Huyu alikuwa na roho ngumu
ikilinganishwa na mimi.

Kwa kweli inasikitisha, wafungwa wengine
walikuwa wanawalilia wenzao siku moja
kabla ya kifo chao.

Lakini wafungwa pia hasa
wale waliohukumiwa kifo, walikuwa katika
hali mbaya zaidi kwa sababu walikuwa
wanasikia jinsi miili inavyodondoka kwenye
kitanzi na wakati mwingine sauti za
maombolezo ya wenzao wakiwa kitanzini.

Yule bwana (aliyekuwa anafanya naye kazi)
alifariki dunia nikatafutiwa mtu mwingine,
lakini hakuweza kuifanya kazi hiyo.
Ilitangazwa tena nafasi hiyo, akapatikana mtu
mwingine akapewa mafunzo, lakini aliifanya
ile kazi kwa siku moja tu, alikimbia na
hakurudia tena kutokana na hofu ya ile kazi,
akapangiwa kazi nyingine.

Hofu aliyokuwa nayo mwenzangu ni sawa na
niliyokuwa nayo nilipoanza kazi hiyo mwaka
1984. Hakika siku ya kwanza kufanya kazi hii
nilipata shida. Nilikuwa naweweseka.
Wale
watu niliowanyonga nilikuwa naona kama
wananikimbiza kwa mashoka, wanasema
‘wewe umetuua wewe’ nawaona kabisa na
sura zao.

Usiku wa siku ile ya kwanza sikulala nilikuwa
napiga kelele hadi mke wangu akaamka. Hali
hii ilinisumbua kwa kipindi kirefu. Wakati
huo baba yangu alikuwa hai, nikamsimulia
jinsi nilivyokuwa naweweseka usiku, baba
alinisaidia kuzunguka na kuhangaika, hali
ikatulia mpaka sasa nipo sawa.

Baba alinitia moyo akisema: “Mwanangu kazi
ni kazi, bora mkono uende kinywani.”
Hata mke wangu hakupenda niifanye kazi hii,
lakini baadaye nilipiga moyo konde na
kuendelea.

*Mwisho ni kilio changu serikalini.* Jamani
mafao ya kustaafu ni kidogo. Naiomba
Serikali ituongezee kidogo na kutukumbuka.

Ilikuwa simulizi iliyojaa hisia tofauti kwetu na ilitufikirisha sana.

Gazeti Mwananchi


USIKOSE HII👉 Usipitwe na Kampeni hii

Endelea kusoma makala hizi zinazofanana na hii ya, Mtu aliyefanya kazi ngumu zaidi afunguka;

a.gif Jiwekee Utaratibu utakaokuwezesha kuamua vizuri juu ya fedha utakazopata

Jiwekee utaratibu utakaokupa uzoefu wa kuamua vizuri juu ya fedha unazopata. Watu tumekuwa tukitumia fedha tunazopata bila kufikiria jinsi ya kugawa ktk matumiz badala yake baada ya kutumia ndio una/ninaanza kujuta Kwa nin nime/umetumia tofauti na mahitaji uliyonayo. Kiasi cha fedha ulichonacho chaweza kukufanya uwe maskini au tajir kutokana na maamuz unayofanya juu ya hiyo fedha. Ukitaka ufanikiwe na ukue kifedha jaribu kugawa fedha uliyopata Kwa mafungu yafuatayo:.. endelea kusoma

a.gif Je, Wewe unayesoma huu ujumbe una ndoto?

KILA mtu duniani ana ndoto ingawa haijalishi ni ndoto gani uliyonayo.
Ndoto uliyonayo ina thamani kubwa kuliko fedha wala kitu chochote kile. Ndoto uliyonayo ina nguvu kubwa ya kubadilisha maisha yako na kukufikisha sehemu ambayo ulitaka ufike ama zaidi ya pale ulipotarajia kufika… endelea kusoma

a.gif Je, unajua kwa nini hufanikiwi?

Una mizigo mingi isiyo ya lazima wala faida ambayo umeibeba:-
1.Umejipa jukumu la kuwa "mpelelezi" wa maisha ya wengine na umesahau maisha yako.
2.Umebeba vinyongo na visasi moyoni vinavyokufanya uwafikirie waliokuumiza zaidi kuliko kufikiria furaha na maendeleo yako… endelea kusoma

a.gif Elimu ya biashara

Jifunze kujikagua, jifunze kujiuliza je hapa ndipo napotakiwa kuwa? Usifurahie tu kwamba upo hapo kwa muda mrefu yamkini unaona panakufaa and you are settled lakini ukweli ni kwamba sio pako na haukutengenezwa kuwa hapo. Hata kama tai ataonekana kwenye banda la kuku lakini ukweli ni kwamba tai kaumbiwa kuwa angani tofauti na kuku aishie bandani. Jiulize hapo ulipo ni pako??.. endelea kusoma

a.gif Jiwekee Utaratibu utakaokuwezesha kuamua vizuri juu ya fedha utakazopata

Jiwekee utaratibu utakaokupa uzoefu wa kuamua vizuri juu ya fedha unazopata. Watu tumekuwa tukitumia fedha tunazopata bila kufikiria jinsi ya kugawa ktk matumiz badala yake baada ya kutumia ndio una/ninaanza kujuta Kwa nin nime/umetumia tofauti na mahitaji uliyonayo. Kiasi cha fedha ulichonacho chaweza kukufanya uwe maskini au tajir kutokana na maamuz unayofanya juu ya hiyo fedha. Ukitaka ufanikiwe na ukue kifedha jaribu kugawa fedha uliyopata Kwa mafungu yafuatayo:.. endelea kusoma

a.gif Kwa nini watu wanapenda pesa

Watu wengi tunapenda sana Pesa lakini hatuko tayari kuzifanyia Pesa kazi nikiwa na maana kutumia njia sahihi kuzipata na tunapozipata hatuna Akili ya kuweza kuwa nazo muda mrefu zisiondoke.
Kama tujuavyo katika maisha yetu haya Pesa ndio kila kitu,tunahitaji Pesa ili tuweze kufanya mambo mengi mazuri na makubwa.Kitu kinachotukwamisha hatujui tufanye nini ili tuweze kuzipata hizi Pesa na tunapozipata tunakosea tena cha kuzifanyia ili zisipotee tena au zisiishe… endelea kusoma

a.gif Ugumu wa maisha huanzia akilini mwako

Ebu fikiria Dada anayechoma mahindi maeneo ya Manzese Darajani kuanzia saa 12 jioni mpaka SAA 2 usiku, kwa siku moja anauwezo wa kuchoma mahindi .50. Kila hindi moja ananunua shambani kwa shilingi 100/- Na Anauza kwa sh.600/-.. endelea kusoma

a.gif Mafanikio ya maisha sio Elimu tuu

MAFANIKIO YA MAISHA SIO ELIMU TU, UTHUBUTU, KUJIAMINI NA UJASIRI WA MAAMUZI.. endelea kusoma

afya-mapishi-na-lishe.png

.

uchumi-biashara-na-ujasiriamali.png
SALAMU-ASUBUHI-987HGZ.JPG
familia-mapenzi-na-mahusiano.png

Website na, Melkisedeck Leon Shine | Tembelea website nyingine Hapa>>.