MASOMO YA MISA, FEBRUARI 10, 2019

JUMAPILI, DOMINIKA YA 5 MWAKA C WA KANISA

MWANZO:

Zab. 95:6-7

Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba; kwa maana ndiye Mungu wetu.

SOMO 1

Isa. 6:1-2a, 3-8

Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita. Wakaitana kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi. Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa. Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 138:1-5, 7-8 (K) 1

(K) Ee Bwana, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.

Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
Nitalishukuru jina lako. (K)

Nitalishukuru jina lako,
Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako,
Kuliko jina lako lote.
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)

Ee Bwana, wafalme wote wa dunia watakushukuru,
Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako.
Naam, wataziimba njia za Bwana,
Kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. (K)

Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu,
Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
Bwana atanitimilizia mambo yangu;
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako. (K)

SOMO 2

1 Kor. 15:1-11

Ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapa mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO

Mt. 8:17

Aleluya, aleluya,
Aliutwaa udahifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu.
Aleluya.

INJILI

Lk. 5:1-11

Ikawa makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao. Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

πŸ™‰πŸ™‰πŸ™‰Usisahau kushare makala hii kuhusu Masomo Ya Ibada Ya Misa Kanisani Leo Jumapili.πŸ‘ Share facebook, twitter n.k bila kusahau WhatsApp!πŸ’―βœ”


IMG_20181021_134248.jpg
Ujumbe wangu kwako kwa sasa

Mungu ni Mwaminifu Sana na mwenye mipango na subira katika kila kitu hasa Sala na maombi yetu kwake. Tunaposali leo Mungu anatusikia na kujibu leo, kesho au hata miaka kumi ijayo. Inawezekana hata baraka zako za leo ni majibu ya Sala zako miaka kumi iliyopita. Sali bila kuchoka kwani hujui Sala zako zitakusaidia lini. Usitegemee majibu ya Sala zako wakati huo huo, amini katika uaminifu wa Mungu kwani anajua lini ni siku sahii ya kukujibu.

Mungu Akubariki sana… Tuombeane!

wadogo.gif

πŸ“š Endelea kusoma kuhusu;-πŸ‘‡

ndugu.gif