NOVENA YA HURUMA YA MUNGU SIKU YA KWANZA

Posted by, Melkisedeck Shine.

NOVENA YA HURUMA YA MUNGU SIKU YA KWANZA, IJUMAA KUU

Novena hii pia inaweza kusaliwa wakati wowote na katika kipindi chochote cha mwaka lakini inapendekezwa kuwa Novena hii ianzwe katika siku ya Ijumaa.

Tujiandae kusali kwa kuanza na sala za awali kama vile Uje Roho Mtakatifu pamoja na Sala ya kutubu kisha tuendelee kama inavyoonyeshwa hapa chini:

Maneno ya Bwana Yesu: β€œLeo niletee WANADAMU WOTE KIJUMLA, HASA WAKOSEFU WOTE. Uwazamishe ndani ya Bahari Kuu ya Huruma yangu. Kwa njia hii utatuliza uchungu wangu kwa ajili ya roho zilizopotea.”

Kiongozi: Tuombe Huruma kwa ajili ya wanadamu wote, hasa kwa ajili ya wakosefu.
Wote: Ee Yesu mwenye Huruma kabisa, ambaye asili yako ni Huruma na Msamaha, usizitazame dhambi zetu, bali utazame tumaini tulilo nalo katika wema wako usio na mwisho. Utupokee sisi sote chini ya ulinzi wa Moyo wako wenye Huruma tele. Usimwache hata mmoja. Tunakuomba hayo kwa njia ya upendo ule unaokuunganisha wewe na Baba na Roho Mtakatifu, katika Umoja wa Utatu Mtakatifu, daima na milele. Amina.

Baba yetu …….. Salamu Maria ……… Atukuzwe …….…
Baba wa Milele, uwatazame kwa macho ya huruma wanadamu wote, na hasa wakosefu maskini, waliongizwa ndani ya Moyo wa Mwanao mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristu, ulio na huruma yako kuu, ili nasi tuisifu na kuitukuza tangu sasa na milele yote. Amina.

Tumia Rozari ya kawaida kusali Rozari ya Huruma ya Mungu kama ifuatavyo:
Baba yetu … Salamu Maria …. X3 Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi …….

Kila penye punje kubwa (Badala ya Baba yetu):
Baba wa Milele, ninakutolea Mwili na Damu, Roho na Umungu, wa Mwanao Mpenzi sana, Bwana wetu Yesu Kristu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zetu, na dhambi za dunia nzima.

Kila penye punje ndogo (badala ya Salamu Maria):
Mwanzishaji: Kwa ajili ya mateso makali ya Bwana wetu Yesu Kristu,

Wote huitika: Utuhurumie sisi na dunia nzima.

Mwisho wa Rozari sali mara tatu sala ifuatayo:

Mungu Mtakatifu,
Mtakatifu mwenye Enzi,
Mtakatifu unayeishi milele,
Utuhurumie sisi na dunia nzima (x3).

LITANIA YA HURUMA YA MUNGU

Bwana utuhurumie – Bwana utuhurumie
Kristu utuhurumie – Kristu utuhurumie
Bwana utuhurumie – Bwana utuhurumie
Kristu utusikie – Kristu utusikilize
Baba wa mbinguni Mungu – utuhurumie
Mwana Mkombozi wa dunia Mungu - utuhurumie
Roho Mtakatifu Mungu - utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu mmoja – utuhurumie.
Huruma ya Mungu iliyo sifa kuu ya Muumba wetu - Tunakutumainia (iwe kiitikio)
Huruma ya Mungu iliyo kilele cha ukamilifu wa Mwokozi wetu
Huruma ya Mungu iliyo upendo usiopimika wa Roho Mtakasa
Huruma ya Mungu fumbo lisilofahamika la Utatu Mtakatifu
Huruma ya Mungu iliyo ishara ya uwezo mkuu wa Mungu Mwenyezi
Huruma ya Mungu iliyofumbuliwa katika kuziumba Roho za Malaika wa mbinguni
Huruma ya Mungu iliyotuumba na kutuamuru tuwepo bila kutokana na chochote
Huruma ya Mungu inayotujalia maisha ya kutokufa
Huruma ya Mungu inayotukinga na adhabu tunazostahili
Huruma ya Mungu inayotuinua tutoke katika taabu, unyonge na maumivu ya dhambi zetu
Huruma ya Mungu inayotufanya wenye haki katika Neno aliyejifanya Mtu
Huruma ya Mungu inayofurika kutoka katika majeraha ya Kristu
Huruma ya Mungu inayobubujika kutoka ndani ya Moyo Mtakatifu wa Yesu
Huruma ya Mungu iliyotupatia Bikira Maria Mtukufu awe kwetu Mama wa Huruma
Huruma ya Mungu iliyoonyeshwa katika kuanzishwa Kanisa Katoliki
Huruma ya Mungu inayopatikana katika mafumbo ya Sakramenti Takatifu
Huruma ya Mungu inayotolewa kwa wanadamu wote kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kitubio
Huruma ya Mungu inayotolewa katika Sakramenti ya Ekaristi na Upadrisho
Huruma ya Mungu inayoonyeshwa kwetu pale inapotuita na kutuingiza katika kuwatakatifuza wenye haki
Huruma ya Mungu inayotimilika katika ukamilifu wa watu watakatifu
Huruma ya Mungu chemchemi ya afya kwa wagonjwa na wote wanaoteseka
Huruma ya Mungu iliyo faraja ya wote wenye uchungu moyoni
Huruma ya Mungu iliyo tumaini la roho zinazosumbuliwa na mkato wa tamaa
Huruma ya Mungu iliyo mwenzi wa daima na popote wa watu wote
Huruma ya Mungu inayowahi kutuletea neema zake
Huruma ya Mungu iliyo amani yao wanaokufa
Huruma ya Mungu iliyo burudisho na faraja yao marehemu wa toharani
Huruma ya Mungu iliyo furaha ya mbinguni kwa watakatifu wote
Huruma ya Mungu iliyo taji la watakatifu wote
Huruma ya Mungu chemchemi ya miujiza isiyokauka

Mwanakondoo wa Mungu uliyetuonyesha huruma yako kuu katika kuikomboa dunia kwa msalaba wako mtakatifu, - utusamehe ee Bwana

Mwanakondoo wa Mungu unayejitolea kwetu kwa mapendo na huruma katika kila adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu,- utusikilize ee Bwana

Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia kwa njia ya huruma yako isiyo na mwisho,- utuhurumie.

Kiongozi : Bwana utuhurumie –
Wote: Kristu utuhurumie, Bwana utuhurumie.
Kiongozi : Huruma anana za Bwana zi juu ya kazi zake zote –
Wote: Huruma za Bwana nitaziimba milele.

Tuombe: Ee Mungu uliye na huruma isiyo na mwisho, na hazina za wema na upendo wako hazina mipaka. Tunakusihi ututazame sisi watu wako huku duniani na kutuongezea huruma yako tena na tena, ili itusaidie tusije tukakata tamaa hata mara moja, haidhuru tukumbane na majaribu makubwa kiasi gani, bali tuweze daima kuzielekea na kuzishika amri zako, kwa matumaini na kutimiza mapenzi yako matakatifu, ambayo ndiyo huruma yenyewe. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristu Mwanao, Mfalme wa Amani na Huruma, aishiye na kutawala nawe, na Roho Mtakatifu, kwa pamoja mkituonyesha huruma, daima na milele. Amina.

.

IMG_20181021_135533.jpg

Ujumbe wangu kwako kuhusu sala

Sala pasipo Imani thabiti, ya nia ya kweli, upendo wa kweli, unyenyekevu wa ndani na tumaini la kweli katika Amani ya rohoni; Haijakamilika na haifai kitu.

Sala ni Hazina. Kusali ni muhimu sana. Sala unayosali leo inaweza kukusaidia hata miaka kumi ijayo au ikasaidia watoto wa watoto wako. Mungu ni mwenye fadhila na anakumbuka yote. Mwombe Mungu akulinde ukiwa mzima ili uwapo hatarini akukumbuke hata kabla hujamwomba.

Mungu Akubariki Daima. Tukumbukane katika sala.

Fwatilia Website hii kwenye Email yako. Ingiza Email yako hapa kisha Bofya SUBSCRIBE na ufuate maelekezo

.

Website na, Melkisedeck Leon Shine | Tembelea website nyingine Hapa>>.