Mafundisho ya Dini

๐Ÿ‘‰Sakramenti ya kwanza daima ni ipi?

Sakramenti ya kwanza daima ni ubatizo, kwa kuwa ndio kupata uzima mpya kwa kushiriki kifo na ufufuko wa Yesu, inavyodokezwa wazi zaidi mtu akizamishwa na kutolewa majini. โ€œTulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzimaโ€ (Rom 6:4). Sakramenti nyingine zote ama zinastawisha ama zinafufua uzima huo wa Kimungu ambao ni sharti la kuingia mbinguni. โ€œAmin, Amin, nakuambia: Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Munguโ€ (Yoh 3:5).

๐Ÿ‘‰Je, ubatizo uliotolewa na Yohane Mbatizaji ulikuwa sakramenti?

Hapana, ubatizo uliotolewa na Yohan Mbatizaji haukuwa sakramenti, kwa sababu yeye alikuwa mtangulizi tu wa Yesu, mwanzilishi wa sakramenti zote. โ€œKweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa motoโ€ (Math 3:11). Paulo aliuliza watu, โ€œโ€˜Mlibatizwa kwa ubatizo gani?โ€™ Wakasema, โ€˜Kwa ubatizo wa Yohaneโ€™. Paulo akasema, โ€˜Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesuโ€™. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesuโ€ (Mdo 19:3-5).

๐Ÿ‘‰Je, watu wazima wanaweza kuelewa sakramenti kwa dhati?

Hapana, watu wazima hawawezi kuelewa sakramenti kwa dhati, kwa kuwa zote ni mafumbo yanayotuzidi. Basi, kama Petro alipooshwa miguu, tumuachie Bwana atufanyie kazi anavyojua yeye. โ€œNifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadayeโ€ (Yoh 13:7). Kisha kuoshwa tuzidi kuchimba mafumbo hayo kwa mwanga wa Neno na wa Roho Mtakatifu. โ€œJe, mmeelewa na hayo niliyowatendea?… Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyoโ€ (Yoh 13:12,15).

๐Ÿ‘‰Sakramenti inayohusiana zaidi na ubatizo ni ipi?

Sakramenti inayohusiana zaidi na ubatizo ni kipaimara, kinachoendeleza kazi yake. โ€œWaliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yaoโ€ (Mdo 19:5-6). Sakramenti hizo ni kama pande mbili za pesa moja. Zinahusiana kama Pasaka na Pentekoste, ambayo ni utimilifu wake, kwa kuwa siku alipofufuka Yesu aliwapulizia Mitume Roho Mtakatifu, ambaye siku hamsini baadaye akawajia kama โ€œupepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yoteโ€ (Mdo 2:2).

๐Ÿ‘‰Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ipi?

Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ekaristi, iliyo kuu kuliko sakramenti zote kwa sababu ndiyo Yesu mzima, Mungu-mtu, katika maumbo ya mkate na divai. Sisi ambao tulishiriki kifumbo kifo na ufufuko wake tukapokea kwake paji la Roho Mtakatifu, tunaalikwa kukaribia mara kwa mara meza anapotulisha na kutunywesha Mwili na Damu yake ili tushiriki uhai wake kwa dhati zaidi na zaidi. โ€œAulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimiโ€ (Yoh 6:56-57). Ubatizo na kipaimara havirudiwi, vinadumu ndani mwetu kama mifupa ambayo ekaristi ya mara kwa mara inazidi kuitia mwili na damu.

๐Ÿ‘‰Daraja na ndoa ni tofauti na sakramenti nyingine kwa sababu gani?

Daraja na ndoa ni tofauti na sakramenti nyingine kwa sababu hazilengi hasa faida ya mtu anayezipokea, bali huduma zake kwa ajili ya Kanisa na jamii. Daraja inatia uwezo wa Kristo kwa ustawi wa Kanisa, Bibi arusi wake. Ndoa inatia upendo wake mwaminifu kwa ustawi wa familia, kanisa dogo la nyumbani. โ€œJitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyeweโ€ (Mdo 20:28). โ€œHakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisaโ€ (Ef 5:29-32).

๐Ÿ‘‰Ndoa ya Wakristo ni sakramenti ya nani?

Ndoa ya Wakristo ni sakramenti ya Yesu na Kanisa lake. โ€œNjoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi arusi, mke wa Mwanakondooโ€ (Ufu 21:9). Wakiwa na ndoa halisi, mume na mke waliobatizwa ni ishara wazi ya hao wanaarusi wawili wasioonekana. โ€œKama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yakeโ€ (Ef 5:24-25). Ndiyo sababu Mkatoliki hawezi kufunga ndoa bila ya kuhusisha Kanisa na kufuata taratibu zake.

๐Ÿ‘‰Sakramenti ni nini?

Sakramenti ni ishara wazi ionekanayo ya neema isiyoonekana, iliyofanyizwa kwanza na Yesu Kristu mwenyewe; ilete neema au izidishe neema moyoni mwetu.

๐Ÿ‘‰Yesu aliweka sakramenti ngapi?

Yesu aliweka sakramenti saba ambazo ni;

1. Ubatizo (Yoh 3:3, Mk. 16:15-16)

2. Kipaimara (Isa 11:2, Mdo 8:14-17)

3. Ekaristi Takatifu (Yoh 6:1-7, 1Kor 11:24-25)

4. Kitubio (Mt 16:18-19; 18:18; Yoh 20:21-23)

5. Mpako Mtakatifu (Mk 6:13, Yak 5:14-15)

6. Daraja Takatifu (Lk 22:21-25; 1Kor 11:24-25)

7. Ndoa (Mwa 2:21-25; Mt 19:3-9)

๐Ÿ‘‰Sakramenti zimegawanyika katika mafungu mangapi?

Sakramenti zimegawanyika katika makundi mawili;

1. Sakramenti za wafu.

2. Sakramenti za wazima.

๐Ÿ‘‰Sakramenti za wafu ni zipi?

Sakramenti za wafu ni Ubatizo na Kitubio. Zaitwa za wafu kwa sababu zinapokewa na watu wasio na neema ya utakaso na zinafufua roho iliyouawa kwa dhambi.

๐Ÿ‘‰Sakramenti za wazima ni zipi?

Sakramenti za wazima ni: Ekaristi Takatifu, Kipaimara, Mpako Mtakatifu, Daraja na Ndoa. Zaitwa za wazima kwa sababu wanaozipokea ni wale wenye Neema ya Utakaso na hivyo huongeza neema rohoni.

๐Ÿ‘‰Sakramenti zipi hutolewa mara moja tuu na kwa nini?

Sakramenti zinazotolewa mara moja tuu ni Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu. Hutolewa mara moja tuu kwa sababu zinachapa alama isiyofutika rohoni. yaanai mtu akiacha imani Katoliki hawezi kuondoa kabisa Sakramenti hiyo.

๐Ÿ‘‰Sakramenti zipi ni kwa ajili ya huduma kwa jamii na kanisa?

Sakramenti zilizowekwa kwa ajili ya huduma kwa jamii na Kanisa ni Daraja Takatifu na Ndoa.

๐Ÿ‘‰Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema zipi?

Kwa Sakramenti ya Kitubio tunapata neema hizi;

1. Maondoleo ya dhambi zote kubwa na adhabu ya milele

2. Maondoleo ya dhambi ndogo na adhabu nyingine za muda (Isa 6:5-7, Yoh 8:11)

3. Twarudishiwa na kuongezewa neema ya utakaso

4. Twasaidiwa kuepa dhambi na twapata nguvu ya kutenda mema

5. Twarudishiwa tena mastahili tuliyopoteza kwa dhambi zetu

๐Ÿ‘‰Sakramenti ya Ekaristi ni nini?

Sakramenti ya Ekaristi ni Sakramenti ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo, aliye kweli katika Maumbo ya Mkate na Divai. (Yoh 6:1-17, Mt 26:26-28)

.

.

Mafundisho

.

Sala

.

.

IMG_20180109_191617.jpg

Kama Una mashaka na Imani na mafundisho ya Kanisa Katoliki soma hapa>>

Website hii inaletwa kwako na Melkisedeck Leon Shine.

Naomba utafakari kuhusu; Kuomba na Kushukuru. Mungu akubariki sana. Tuombeane…!