Katika maungamo ni lazima kuwa wanyenyekevu na wanyofu. Shetani daima anatuwekea mtego wa aibu, ni lazima tuutegue. Baadhi ya aibu anazotuwekea shetani ni pamoja na:

Mtego wa kwanza ambao shetani anatuwekea: Muungamishi wangu atanigombeza nikisema dhambi hii: Jiulize -Kwa nini akugombeze? Muungamishi anayegombana na mfanya toba anayekuja kujitakasa na kuinuliwa toka tope la dhambi hafai. Muungamishi anapaswa kuonesha upendo kwa wote wanaokuja katika kiti cha huruma ya Mungu.

Upo utani unaodhihirisha vigezo ambavyo wengi wetu tunajiwekea ama kwa kufahamu au kwa kutokufahamu. Vigezo vyenyewe ni kwamba:

Muungamishi wangu sharti:
👁awe mzee,
👁asiwe na kumbukumbu nzuri,
👁asiwe anasikia vizuri,
👁asiwe anaona vizuri,
👁awe anasinzia wakati kuungamisha.

Mmoja anapofika kwenye kiti cha huruma ya Mungu akigundua kwamba muungamishi hana vigezo hivyo utaona jinsi anavyokurupuka kutaja dhambi kama cherehani, anavyopunguza sauti na anavyohitimisha ungamo lake. Hapo hakuna ungamo ila kufuru la ungamo.

Wengi wetu tunafikiri kwamba sakramenti ya upatanisho huanzia kwenye kiti cha maungamo. Mchakato ulishaanza ulipoguswa na Neema ya toba, tangu ulipotoka nyumbani. Kinachohitajika sasa ni utulivu na kuungama, ili kupata uponyaji wa kweli na upokee ushauri unaoendana na hali yako.

Mtengo wa pili: Wapo wanaosema Muungamishi wangu atakwazika kwa dhambi hii na atanichukia: hakika huu nao ni uongo uliotopea na kukubuhu, kwa nini akakwazike ila atafurahi kuona kuwa upo tayari tena kurekebisha hali yako ya ndani. Hutakuwa wa kwanza wala wa mwisho kuungama dhambi hiyo. Hawezi kukuchukia, zaidi ya hayo atakuwa msaada mkubwa ili kubandukana na dhambi hiyo.

Mtego wa tatu: Siendi kuungama leo mpaka aje Padre mgeni: Kuahirisha: Baadhi ya watu hawana umakini katika maisha yao ya kiroho. Wanaendelea kuahirisha suala la kumchagua Mungu ingawa kila mara wanapewa changamoto na Neno la Mungu, mafundisho ya Kanisa, mapokeo ya Kanisa, maisha ya Watakatifu na kutoka dhamiri zao wennyewe. Hawa ni kama Bata, ambaye ingawa amezamishwa katika maji kwa masaa, wanapotoka kwenye maji hawaruhusu maji kugusa manyoya yao.

Wengi walioingia katika kishawishi hiki, badala ya kuepuka dhambi wanaendelea kupokea, na kukufuru. Kufuru ni dhambi kubwa. Wanageuza damu ya Yesu kuwa sumu kwao. Hebu tujiulize ni nini kitatokea katika kifo cha ghafla, kitokanacho na ajali au magonjwa?

Mtego wa tatu: Siwezi kuungama kwa Padre huyu kwani maisha yake si mfano bora. Naye ni mdhambi na mwingi wa kashfa. Haya ni makwazo: wapo baadhi ya watu ambao hawaoni sababu ya wongofu kwani wanakwazwa na wale ambao wanadhaniwa wamekwisha ongoka, hususani mapadre na watawa lakini wanaishi maisha mabaya na ya dhambi.

Mt. Fransisko wa Assisi anasema hivi: “Hata kama ningefahamu kashfa nyingi kiasi gani kuhusu Padre fulani nitampa heshima kubwa kuliko ningekutana na malaika kwani yeye amewekwa wakfu, na ni katika yeye tunaweza kuadhimisha Misa Takatifu na maadhimisho mengine ya sakramenti za wokovu, uwezo ambao malaika hawakupewa, tunachopaswa kufanya siyo kuwahukumu bali kuwaombea kwa Mungu. Wewe ni nani hata umhukumu mwenzio?

Ndugu zangu, tusikubali dhambi itutawale. Matokeo ya dhambi kututawala yanaonekana katika maneno ya mzaburi: “Dhambi huongea na mtu mwovu, ndani kabisa moyoni mwake, wala jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake” (rej. Zab 36:1).

Tuwe wanyenyekevu kama Mzaburi anavyotushauri. Sisi sote ni wadhambi – tuungame na kuomba Neema ya Mungu kwa unyenyekevu: “Lakini ni nani ayaonaye makosa yake mwenyewe? Ee, Mungu uniepushe na makosa yale nisiyoyajua, unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi, usikubali hayo yanitawale.” (rej. Zab 19:12-13).

Mt. Gregor alizoea kusema kuwa dhambi inakuwa katika ngazi tatu:
👉🏾Kushawishiwa kutoka kwa shetani. Kwa kufikiri furaha utakayopata:
👉🏾kutoka katika miili yetu. Kukubali:
👉🏾Kutoka katika akili zetu na utashi wetu

Mt. Augustino alisema kuwa: “Hakuna mtu anayetenda dhambi kwa kosa ambalo hawezi kulikwepa.” Tegua mtego wa shetani kabla hajakunasa.

Shetani anapata wafuasi wengi kwa kufundisha kuwa dhambi ni kitu kibaya. Anawaaminisha wafuasi wake kuhusu ubaya wa dhambi, baadaye anawachanganyisha na kuwasadikisha kuwa Mungu hatajali sana dhambi zao.

Baadaye wakishasahau dhambi zao, wanaendelea wakitenda dhambi maisha yao yote wakifikiri juu ya ubaya wa dhambi za wengine. Ndiyo maana watu wengi hawapendi kuongelea juu ya dhambi na mapungufu yao, bali hufurahia umbea, uzushi, masengenyo, kuchokonoa, kushabikia na kushutumu wengine kuhusu dhambi na mapungufu yao.

Yesu anasema kuwa, “Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni BORITI iliyo jichoni mwako?…mnafiki wewe! Ondoa kwanza Boriti iliyoko jichoni mwako, ndipo utaona waziwazi kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichoko jichoni mwa mwenzako.” (rej. Mt 7:3,5).

Sakramenti ya upatanisho ni kwa ajili yetu, tumepewa na Kristo kwa ajili ya uponyaji wa nafsi zetu. Lakini pasipo kuungama, kukiri uwepo wa Mungu, na hitaji letu la huruma na msamaha wake, hapawezi kuwapo na uponyaji. Ndio maana Mwinjili Yohani katika nyaraka zake anasisitiza kwamba: “Tukisema kwamba hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe na ukweli haumo ndani yetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu, na kututakasa na uovu wote.” (rej. 1Yn 1:8-9).

Fr. Innocent Bahati Mushi OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)

🙉🙉🙉Usisahau kushare makala hii kuhusu Mitego ya Shetani katika maungamo.👍 Share facebook, twitter n.k bila kusahau WhatsApp!💯✔


IMG_20181021_134131.jpg
Ujumbe wangu kwako kwa sasa

Sala siyo maneno mazuri, bali sala ni NIA ya Upendo iliyobebwa na maneno mazuri. Tusali kwa kunuia kutoka moyoni na sio kwa kunena maneno tuu mdomoni.

Mungu Akubariki sana… Tuombeane!

baada-ya-kufa.JPG

📚 Endelea kusoma kuhusu;-👇

Slide1-mabest-skull.PNG