MASOMO YA MISA, MACHI 20, 2016
DOMINIKA YA MATAWI NA KUKUMBUKA MATESO YA BWANA

SOMO 1

Isa 50:4-7
Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang'oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu

WIMBO WA KATIKATI
Zab 22:7-8, 16-17a; 18-19, 22-23

(K)Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

Wote wanionao hunicheka sana,
Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;
Husema, Umtegemee Bwana; na amponye;
Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. (K)

Kwa maana mbwa wamenizunguka;
Kusanyiko la waovu wamenisonga;
Wamenizua mikono na miguu.
Naweza kuihesabu mifupa yangu yote. (K)

Wanagawanya nguo zangu,
Na vazi langu wanalipigia kura.
Nawe, Bwana, usiwe mbali,
Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia. (K)

Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu,
Katikati ya kusanyiko nitakusifu.
Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni,
Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni,
Mcheni, enyi nyote mlio wazao wa Israeli. (K)

SOMO 2
Flp 2:6-11

Kristo Yesu ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

INJILI
Lk 22:14- 23:56

Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu yalivyoandikwa na mtakatifu Luka.

Karamu ya Pasaka
Hata saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye. Akawaambia, Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu. Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja.

Yesu anaweka Ekaristi Takatifu
Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.] Walakini, tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani, Kwa kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule amsalitiye! Wakaanza kuulizana wao kwa wao, ni yupi miongoni mwao atakayelitenda jambo hilo.

Ni nani mkubwa?
Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye. Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi; mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.

Yesu anatabiri kano la Petro na wongofu wake
Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui.

Ni saa ya mkataa kupigana na shetani
Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La! Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho yake akanunue. Kwa kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa, Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake. Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi.

Katika bustani ya Gethsemane
Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye. Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.] Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni. Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni.

Yesu anakamatwa
Basi alipokuwa katika kusema, tazama, mkutano wa watu, na yule aitwaye Yuda, ambaye ni mmoja wa wale Thenashara, amewatangulia. Akamkaribia Yesu ili kumbusu. Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu? Na wale waliokuwa karibu naye walipoona yatakayotukia, walisema, Bwana, tuwapige kwa upanga? Mmoja wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Yesu akajibu akasema, Mwe radhi kwa hili. Akamgusa sikio, akamponya. Yesu akawaambia wakuu wa makuhani, na maakida wa hekalu, na wazee, waliokuja juu yake, Je! Mmekuja wenye panga na marungu kama kukamata mnyang'anyi? Kila siku nilipokuwa pamoja nanyi hekaluni hamkuninyoshea mikono, lakini hii ndiyo saa yenu, na mamlaka ya giza.

Kano la Petro
Wakamkamata, wakamchukua, wakaenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Na Petro alimfuata kwa mbali. Na walipokwisha washa moto katikati ya kiwanja, waliketi pamoja, naye Petro akaketi kati yao. Ndipo mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia macho akasema, Na huyu alikuwa pamoja naye. Akakana, akisema, Ee mwanamke, simjui. Baadaye kitambo mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao. Petro akasema, Ee mtu, si mimi. Halafu, yapata saa moja, mtu mwingine alikaza kusema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya. Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema, jogoo aliwika. Bwana akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile neno la Bwana jinsi alivyomwambia, Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu. Akatoka nje akalia kwa majonzi.

Dhihaka na matukano
Na wale watu waliokuwa wakimshika Yesu walimfanyia dhihaka, wakampiga. Wakamfunika macho, kisha wakamwuliza-uliza wakisema, Tabiri, ni nani aliyekupiga? Wakamtolea na maneno mengine mengi ya kumtukana.

Yesu mbele ya baraza kuu ya Kiyahudi
Hata kulipokucha, walikutanika jamii ya wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, wakamleta katika baraza yao, wakisema, Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie. Akawaambia, Nijapowaambia, hamtasadiki kabisa. Tena, nikiwauliza, hamtajibu. Lakini tangu sasa Mwana wa Adamu atakuwa ameketi upande wa kuume wa Mungu Mwenyezi. Wakasema wote, Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu? Akawaambia, Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye. Wakasema, Basi, tuna haja gani tena ya ushuhuda? Maana, sisi wenyewe tumesikia maneno ya kinywa chake.

Yesu mbele ya Pilato
Wakasimama mkutano wote, wakampeleka kwa Pilato. Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema. Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na makutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu. Nao walikaza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi yote, tokea Galilaya mpaka huku.Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya. Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile.

Yesu mbele ya Herode
Na Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akataraji kuona ishara iliyofanywa na yeye. Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lo lote. Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana. Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato. Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao.

Yesu mbele ya Pilato tena
Na Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu, akawaambia, Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki; wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilolitenda lipasalo kufa. Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [Maana ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.] Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba. Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu. Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulibishe. Msulibishe. Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua. Lakini wakatoa sauti zao kwa nguvu sana, wakitaka asulibiwe. Sauti zao zikashinda. Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike. Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo.

Yesu anajitwika msalaba kwenda Golgota
Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu. Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea. Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu? Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye.

Yesu anasulibiwa
Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.

Wanamdhihaki na kumtukana Yesu msalabani
Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.

Mhalifu mmoja anapata msamaha
Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.

Kifo cha Yesu
Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. Alipokwisha kusema hayo alikata roho.

Baada ya kufa kwake Yesu
Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki. Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipiga-piga vifua. Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.

Yesu anazikwa
Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki; (wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu; mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake. Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia. Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa. Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

πŸ„πŸΎπŸ™πŸ„πŸΎπŸ•Š

HURUMA-YA-MUNGU.png