Ukeketaji ni nini?

Katika baadhi za jamii viungo vya uzazi vya nje vya msichana,
yaani kisimi au sehemu ya ndani na nje ya mashavu ya uke
yanakatwa na kuondolewa kabisa. Huu ndiyo ukeketaji au
kutahiriwa kwa mwanamke.
Wakati mwingine uekeketaji hufanyika katika umri wa miezi ya
mwanzo ya maisha ya mtoto wa kike. Mara kwa mara kutahiriwa
kwa wanawake hufanyika wakati msichana anapofikia utu uzima
au kuadhimisha na kuvuka kutoka utoto kuingia utu uzima.
Mara nyingine ukeketaji ni sehemu ya unyago na kuadhimia kwa
msichana kujifunza jinsi ya kuwa mtu mzima.
Kuna aina mbalimbali za ukeketaji:
1 Sehemu ya ngozi inayofunika kisimi huwa inaondolewa.
Mara nyingine kisimi au eneo lake hukatwa pia. Watu
wengi huita aina hii sunna.
2 Kisimi pamoja na sehemu za mashavu ya ndani
hutolewa.
3 Sehemu yote au baadhi ya viungo vya nje hutolewa na
uke hufungwa kwa kushona. Hii huacha sehemu ndogo
ya tundu ambapo mkojo na damu ya mwezi (hedhi)
hupita. Aina hii huitwa mfyato (Infibulation).
4 Aina yeyote ya kuchezea kwa lengo la kuharibu
sehemu yoyote ya viungo vya nje kama vile kutia vitu
vyenye madhara kwenye uke, kurefusha mashavu au
kisimi kwa kuvivuta au kutoboatoboa.