Sherehe na tarehe ya Kuzaliwa kwa Yesu Kristo

By, Melkisedeck Shine.

TAREHE YA KUZALIWA KWA KRISTO

by Fr TITUS AMIGU

Nimeombwa nifafanue tarehe ya kuzaliwa Yesu Kristo kama ni kweli ni tarehe 25 Desemba au la.
Lakini kwa ajili ya kuwekana sana nimeyagundua maswali mawili yanayoweza kufuata baada ya kujibu swali hili la msingi. Ndiposa nimeambatanisha majibu kwa maswali hayo ya nyongeza. Swali moja ni kwa nini tunaadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo kila mwaka na lingine ni Yesu alitungwa mimba lini. Nifuatilie.
Nitaanza kujibu swali la kwa nini tunaadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo kila mwaka, kisha nitajibu swali la tarehe ya kuzaliwa Yesu Kriisto na kumalizia na swali la Yesu alitungwa mimba lini. Mpangilio huu unasababishwa na mantiki ya majibu yenyewe.

1. Kwa nini tunaadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo kila mwaka?

Najibu kifupi. Tunaadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo kila mwaka kwa ajili ya kujichumia faida zake ya kiroho na maadhimisho yenyewe si suala la kumzalisha Yesu tena na tena isipokuwa kuliishi upya tukio hilo kila mwaka. Hivi, tunapoadhimisha Krismasi si kwamba Yesu Kristo anazaliwa upya kila mwaka, isipokuwa tunakumbuka upya kuzaliwa kwake. Ni kumbukumbu (anamnesis).
Narudia, tunachofanya si kumzalisha upya Yesu Kristo kila mwaka isipokuwa ni kuliadhimisha tukio upya au kulikumbuka upya tukio (anamnesis). Tukio hilo lilikuwa muhimu kwa vile mtoto aliyekuwa anazaliwa alikuwa anakuja kuwa shujaa wetu.
Haiwezekani kumzalisha Yesu kimwili kila mwaka na ndivyo isivyowezekana kwa binadamu yeyote. Yesu alikuwa Mungu - Mtu lakini alikuwa mwanadamu kweli na siyo mcheza « Ze comedy » fulani. Kwa ukweli huo, bila shaka, tunajua wote kwamba Yesu, kama binadamu wa kweli, alizaliwa hapa duniani mara moja tu. Aghalabu, tunajua kwamba Yesu hatazaliwa tena na ndiyo kisa tunasubiri kurudi kwake mara ya pili kwa vindumbwendumbwe vya kiyama, ufufuko wa wafu na hukumu ya pili kwa kila mwanadamu. Kwa hilo, tumetahadharishwa wote tukae chonjo: tukeshe usiku na mchana, tujiandae kwa kuishi kwa imani isiyo na mawaa na utendaji wa kiadilifu huku tukiikimbia dhambi kama ukoma.

Kumbe, kuadhimisha tukio upya au kulikumbuka upya tukio siyo KULITUKIZA upya tukio. Acha nikupeni mifano miwili. Kuadhimisha upya tukio la uhuru wa nchi au kukumbuka upya siku ya kupata uhuru si kupata uhuru kwa mara nyingine. Kuadhimisha upya tukio la kufunga ndoa au kukumbuka upya siku ya kufunga ndoa si kufunga ndoa kwa mara nyingine.Vivyo hivyo, kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo fulani si kumzalisha upya.
Si siri, Noeli au Krismasi ni siku ya kuzaliwa shujaa wetu. Siku ya kuzaliwa Mkombozi ni karibu nusu ya ukombozi wenyewe. Au sivyo? Ndiyo kisa basi, furaha haiwezi kuzuiliwa na mtu yeyote wala kwa sababu yoyote. Ni lazima kuifurahia sikukuu ya mtu wa maana hivyo. Mtu asiyeweza kuifurahia siku kama hiyo kuna mawili: ama ni mwendawazimu asiye na habari na mambo ya maana duniani au ni mfanyakazi wa kwenye kiwanda cha sumu. Vinginevyo, mtu mwenye akili timamu na anayefanya kazi za kawaida za kibinadamu sharti afurahi sana.

2. Tarehe ya Kuzaliwa Yesu

i. Tarehe ya Kiblia Ipo

Ili kukata maswali yafaa tuanzie masafa haya.

Watu wengine huhaha huko na huko kutafuta tarehe aliyozaliwa Yesu wakati imeandikwa waziwazi kwenye Maandiko Matakatifu. Imeandikwa, usinibishe. Luka anataja tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu waziwazi, ilikuwa ni mwaka ule Kaisari Augustino alipotangaza sensa, yaani ile sensa ya kwanza katika enzi za ugavana wa Kwirinus huko Siria.
Imeandikwa: “Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote nchini kote wahesabiwe. Sensa hiyo ilikuwa mara ya kwanza, wakati wa Kwirinus alipokuwa gavana wa Siria. Basi, wote waliohusika walikwenda kuhesabiwa kila mtu katika mji wake. Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya, na kwa vile alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi, alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yudea, alikozaliwa mfalme Daudi. Alikwenda kuhesabiwa pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mjamzito. Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia, akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni” (Lk 2:1-7). Umeilewa tarehe hiyo?
Sisi tunaweza kubabaika sana juu ya tarehe hii, kumbe kwa watu wa wakati ule, tarehe hii ilikuwa wazi kama mchana. Ilikuwa ni sawa na kusema huku kwetu, mtoto huyu alizaliwa mwaka ule lilipofunguliwa daraja la Kigamboni, Mheshimiwa Paulo Makonda alipokuwa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Rais John Pombe Mgufuli. Kwetu tarehe hii ni wazi kabisa, yaani mwaka 2016, lakini baada ya karne nyingi kupita tarehe hii iliyo wazi inaweza kuwa jambo la kubishaniwa sana.

Jambo hili si geni kwetu sisi Waafrika. Anayestaajabu anatustaajabisha wenzake. Waafrika hatukujua kusoma wala kuandika. Hatukuwa na kalenda yenye kueleweka. Hivi si haba Waafrika ambao wakiwauliza wazazi wao tarehe walipozaliwa wanaambiwa mathalani, “Ulizaliwa mwaka wa neema kubwa ya maboga alipotutembelea mjomba wako”. Au “Ulizaliwa mwaka wa nzige wengi nasi tufikwa na njaa kali sana” na kadhalika. Ajabu iko wapi?
Kumbe, sisi sote tukipekua na kutaka kujua tarehe kamili ya kuzaliwa Yesu, kama aliyotuandikia Mwinjili Luka, tunaishia kupata kizunguzungu na kubishana tu. Hata hivyo, duniani si wote tunaoshindwa hesabu. Kumbe, zamani zile, kwa misingi ya tarehe ya kuzaliwa Yesu, Wakristo walishatengeneza kalenda.

ii. Tatizo la Kalenda ya Dunia

Lakini katika kuitumia kulitokea haja ya kuirekebisha.
Watu wa kale waliikalia chini kalenda yao. Katika kuirejea wakagundua mushkeli fulani. Waliona kulishafanyika makosa ya miaka minne au sita hivi, yaani kwamba kalenda yao ilitindikiwa miaka minne au sita hivi.

Kasoro hiyo waliigundua pale walipopambanisha miaka ya utawala wa Mfalme Herode Mkubwa na Yesu.
Waliona wameanzia kuhesabu kwenye mwaka wa mbele zaidi wakati walitakiwa kuanzia nyuma miaka minne au sita hivi. Waligundua kwamba walipaswa kurudisha nyuma miaka ya kuzaliwa Yesu hadi ikutane na utawala wa Mfalme Herode Mkubwa. Maana yake kwa kadiri ya kalenda yao, Kristo alizaliwa mapema kuliko mwaka ule iliposemekana kwa ujumla kwamba alizaliwa.

Udadisi wao ulianzia kwenye matumizi ya jina “augustus” linalotajwa na Luka katika 2:1-7. Kumbe, jina hilo ‘augustus’ lenye maana ya “mheshimiwa” kwa Kilatini, ni jina ambalo Gaius Octavius alijipa mnamo 27 K.K. Huyu alikuwa mtawala wa Dola ya Rumi, yaani Kaisari (Mfalme) tangu 31 K.K. mpaka 14 B. K. Na tena, Herodi Mkubwa anayetajwa kutaka kumuua Kristo, alikufa mnamo mwaka 4 K.K. Hivi kuipanga kalenda yao kwa kusema, Yesu alizaliwa mwaka 1, kwa pale walipoanzia hesabu zao, yaani mwaka wa kuanza mji wa Roma, ilimaanisha kuzisahau tarehe hizi muhimu. Wakawa wameisahau miaka minne au sita nyuma.
Walijilaumu kwa kosa hilo kwani iliwapasa wakati ule ule kurudi nyuma kwa miaka michache, ili Yesu azaliwe kabla Herode Mkubwa hajafa. La sivyo, uadui wao usingelikuwapo.

Kwa maelezo haya ya kosa walilofanya wapanga kalenda wa awali zile, mwaka huu 2016 ulipaswa uwe mwaka 2020 au 2021 au 2022. Kwa vyovyote, licha ya kuligundua kosa hilo la miaka minne au sita waliiacha kalenda yao iendelee. Na ndiyo kalenda inayoendelee hadi leo hii. Hii ndiyo kalenda iliyotupatia mwaka huu kama mwaka 2016 na hivi karibuni tutaingia mwaka 2017 badala ya mwaka 2021, 2022 au 2023. Si kitu, twende tu.
Mwenye ubavu wa kiakili, atusaidie kujenga kalenda mpya. Kama unaweza wewe kuitafsiri tarehe aliyozaliwa Yesu na kuipangia kalenda kamilifu jaribu! Lakini nadhani itakuwa kazi isiyo na tija yoyote. Zaidi ya hayo, tusahihishe kalenda leo kwa faida gani au kwa faida ya nani? Acha tuendelee tu!

Je, mnastaajabu? Msistaajabu. Basi, tangu zamani kulikuwa na ugumu wa kupata mwaka aliozaliwa Yesu, sembuse siku na saa. Lakini, pamoja na ugumu huo wa kupata mwaka, mwezi, tarehe na saa kamili alipozaliwa Yesu, ni ukweli usiopingika kwamba, Yesu alizaliwa kama mtu. Ukweli huu hautegemei kujua kwetu mwaka, mwezi, siku na saa. Ni ukweli wa milele,

iii. Hitaji la Kusherehekea Kuzaliwa kwa Mkombozi

Tunaambiwa kwenye Biblia kwamba siku yoyote aliyoifanya Bwana lazima tuisherehekee na kuifurahia. Siyo siku kama siku isipokuwa kile kilichofanywa na Bwana. Unabisha? Bila shaka utanibisha mimi kwa vile hujishughulishi na usomaji na upembuzi wa Maandiko Matakatifu. Basi, kama huna habari imendikwa kwa wino mweusi hivi: “Hii ndiyo siku aliyoifanya Mwenyezi Mungu, tuishangilie na kufurahi” (Zab 118:24). Ndipo likaja swali tusherehekee lini kuzaliwa kwa Mwokozi wetu au kufufuka kwake? Tukio la kuzaliwa kwake ni la thamani kubwa!

iv. Uamuzi wa Utamadunisho

Lakini hapa tuongelee tarehe ya tukio la kuzaliwa tu.
Hilo la kufufuka tuliweke pembeni. Kama unakubaliana nami kwa ushuhuda huo, lilibaki deni la kuzipata siku za Mungu, na hapa hiyo siku aliyozaliwa Bwana wetu ili tuishangilie na tuifurahie. Jiulize, haki na wajibu huo tungalitimizaje bila kuitafuta siku aliyozaliwa Yesu Kristo?
Basi, kwa haki waamini walitafiti tafiti mazingira yao, kwa akili waliyokirimiwa na Mungu, ili kupata siku moja waamini wapate kusherehekea kuzaliwa Yesu Kristo. Mwishoni mwa tafiti yao, wakaigundua siku ya kufaa, ndiyo tarehe 25 Desemba. Hivi, kifupi, hii haina maana kuwa 25 Desemba ndio siku kamili alipozaliwa Kristo, ila imewekwa hapo kwa sababu za kihistoria na utamadunisho uliohalalishwa. Tena ingeweza kuwa tarehe nyingine yoyote kwa sababu HATUADHIMISHI SIKU bali TUKIO LA KUZALIWA YESU. Tuelewane hapa. Hatuadhimishi tarehe 25 Desemba isipokuwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Kwa kuwa tunababaishana sana hapa duniani, yafaa leo tupitie historia hiyo japo kifupi. Hata hivyo, kwa kuwa ninayotaka kukueleza hapa yatahusisha namba na hesabu hesabu, jiandae kwa kukishikilia kichwa chako vyema kisije kikaanza kushika moto na kuwaka kwa maumivu yasiyotibika kwa dawa ya maumivu ya dawatatu. Naomba tufuatane kwa karibu sana.
Ni hivi, katika siku za mwisho za dola ya kipagani ya kirumi, ibada za kuabudu jua zilikuwa zikifanyika sana. Mjini Roma dini ya Mithras, mungu - jua wa kiajemi, ilistawi sana. Kaisari Aureliani akajengesha hekalu la jua lisiloshindika, mnamo mwaka 274. Sikukuu kubwa ya mungu - jua, ilifanyika kila tarehe 25 Desemba, siku ambayo tabia ya kupungua pungua kwa mwanga wa jua ilikoma, na hivyo kuanza kuongezeka tena. Yaani, ilikuwa kama siku ya kuzaliwa upya jua. Na tangu tarehe hiyo, siku zilianza kuwa ndefu tena.

Mambo haya ya kupungua na kuongezeka kwa mwanga wa jua, ndiyo yanayotokea huko Ulaya kila mwaka hadi leo hii. Basi, sikukuu hiyo ya jua iliitwa siku ya kuzaliwa jua lisiloshindika, maana ijapo mwanga ulikuwa ukipungua, jua lilikuwa halifi kabisa.
Tangu siku za Kaisari wa kwanza mkristo, Kostantino, tarehe ya sikukuu ya mungu - jua ikafanywa sikukuu ya kuzaliwa Bwana Yesu Kristo, Mungu asiyeshindika kweli badala ya jua, kiumbe chake mwenyewe. Wayahudi walishindwa kummaliza Yesu, alifufuka mzima. Tunajua kwamba hata jua halikupata kuwako bila NENO (Yn 1: 1- 3).
Tukisoma Kalenda ya Mashahidi iliyotengenezwa na Philocalus mnamo mwaka 354, tunaweza kuona kwamba, sikukuu ya kwanza ya Krismasi ilisherehekewa mwaka 336 huko mjini Roma. Katika kalenda hii, Krismasi iliwekwa mwanzoni mwa mwaka wa liturujia.

v. Sababu Tatu za Tarehe 25 Desemba

Yaonekana kulikuwa na sababu tatu zilizosababisha kuwekwa kwa sikukuu ya kuzaliwa Bwana hapo 25 Desemba.

Mosi, mkazo wa kiteolojia kwenye kitendo cha Yesu kujifanya mtu, kujimwilisha, yaani kuadhimisha kanuni ya imani ya Nicea (mwaka 325) kimatendo na kikamilifu zaidi. Ni kanuni hii ya imani na si ile fupi ya mitume, iliyokazia fumbo la Yesu kujifanya mtu kama sisi.

Pili, kumtambua Kristo kama mwanga wa kweli, jambo linalosemwa na Mal 4:2. Basi, Kaisari Kostantino hakuona ni vibaya sikukuu ya Yesu aliye mwanga, ikichukua nafasi ya sikukuu ya mungu - jua, kwa vile mwenyewe alikuwa mwabudu jua hapo mwanzo kabla hajabatizwa.

Tatu, ujenzi wa kanisa la Mt. Petro pale Vatikani. Ujenzi wa kanisa hilo ulikuwa mgumu. Kwa nia ya kujenga juu ya kaburi la Mt. Petro, ilipasa watu wabomoe nusu mlima. Na hapo karibu na kaburi kulikuwa na altare ya mungu - jua, ambayo nafasi yake ilichukuliwa na altare ya kutolea sadaka ya kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo.

vi.Krismasi Ilichelewa Mashariki

Kwa upande wa mashariki mwa dunia iliyojulikana wakati ule sherehe ya Krismasi ilifika baadaye kidogo:
- Siria kati ya 363 na 373 kwa ushuhuda wa nyimbo za Ephrem,
- Kostantinople mnamo 380 ambapo Gregory wa Nazienzi alihubiri kwamba Krismasi ni matukio ya Bwana kujifanya mtu na kuzaliwa kwake, taarifa ya malaika kwa wachungaji, kutolewa Bwana hekaluni alikokutana na Simeon na Anna na kutembelewa kwake na mamajusi. Gregory alihubiri kwamba, Tokeo la Bwana maana yake hasa ni Ubatizo wa Bwana, mwanga wa dunia.
- Antiokia, Krismasi ilianza mwaka 386, Misri mwaka 432, Yerusalemu kati ya 424 na 458, n.k.

vii. Tarehe Tofauti Tofauti

Kutokana na migogoro ya kihistoria, makanisa ya magharibi yameachana njia na makanisa ya mashariki.
Makanisa hayo ya mwanzo hutenganisha Krismasi (25 Desemba) na Tokeo la Bwana (6 Januari), wakati yale ya mashariki, yaani makanisa ya kiorthodosi husherehekea yote bila kutenga kila tarehe 6 Januari.
Kifupi, tarehe ya kuadhimisha katika Kanisa la Magharibi na baadhi ya Makanisa ya Mashariki pamoja na walimwengu wengine ni tarehe 25 Desemba. Lakini katika baadhi ya Makanisa ya Mashariki huadhimishwa tarehe 7 Januari. Na katika makanisa ya Kiarmeni huadhimishwa tarehe 6 Januari.

Mgawanyiko huu ni wa watu. Biblia inasema kimoja tu kwamba, Kristo alizaliwa (rej. Lk 2:1-7) na akawaletea watu utukufu wa Mungu. Tarehe si jambo la kukosea usingizi. Unabisha? Unabisha nini? Hivi, ikiwa hujui siku aliyozaliwa babu wa babu yako inamaanisha hakuzaliwa na hakuwapo? Usitake nicheke ukayaona mapengo yangu mie!

viii. Je, Tarehe ni Muhimu Sana?

Tujiulize sote. Hivi, hatuwezi kumwamini Kristo mpaka tujue alizaliwa lini? Je, tunaweka kumbukumbu za tarehe za matukio yetu muhimu? Je, tunazo sikukuu zo zote za kale ambazo tunaweza kuzitamadunisha kwa kupisha sikukuu za kikristo? Je, viongozi wetu wakristo wanaweza kutusaidia nini katika kupanga liturujia yetu? Kaisari Konstantino aliwasaidia sana wakristo wenzake. Tunapowaombea viongozi wetu wajali dini zetu tunataka wafanye nini? Tunataka wasifanye chochote? Mbona Konstantino alifanya na sasa analaumiwa?

3. Tarehe ya Kutungwa Mimba Yesu Kristo

Baada ya kulijibu swali la tarehe ya kuzaliwa Yesu Kristo, nadhani sasa tunaweza kujibu swali dogo zaidi, “Bikira Maria alipata mimba lini?” Kwa maneno mengine swali dogo ni Yesu alituungwa mimba lini?
Pasipo mashaka yoyote, kwa vile Yesu alikuwa mwanadamu halisi, alichukuliwa kwenye mimba kama mwanadamu halisi yaani kwa miezi tisa vile vile. Biblia inataja tarehe ya kutungwa kwake sawia na tarehe ya kuzaliwa kwake.
Hata hivyo, tarehe ya kutungwa mimba ya Yesu Kristo kumetajwa kwa tarehe inayotupasa kuielewa vyema. Biblia inatuambia ilikuwa ni mwezi wa sita, malaika Gabrieli alipotumwa kumwendea mwanamwali Bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo lilikuwa Mariamu (rej. Lk 1:26-27).
Hata hivyo, mwezi huu wa sita si kwa hesabu za kuanzia mwanzoni mwa mwaka, isipokuwa kwa hesabu ya ujauzito wa Elizabeti, mke wa mzee Zakaria. Aya 26 inaendeleza yaliyosemwa kabla yake yaani kwamba Elizabeti alipata mimba yake uzeeni (rej. Lk 1:23-25). Hivi basi ni mwezi wa sita kwa mimba ya bi mkubwa huyo na si mwezi wa kizungu Juni.
Watu wanapoelewa mwezi wa sita kuwa mwezi wa kizungu Juni, hushikwa na homa wanapoona Wakristo wakisherehekea kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo mwezi Desemba. Hao huchanganyikiwa kwa mikokotoo ya hesabu zao batili kwa kiasi kile zilivyoegemezwa kwenye mwezi walioukosea.
Wachache hawaiendi mbali ya kuajabia. Lakini wengine hudhani, kwa kituko hicho kwamba Yesu alizaliwa “njiti”. Na hapo ndipo wengine huenda kwenye kosa kubwa zaidi la kudai Yesu alikuwa mtu wa pekee kwa vile alikaa tumboni mwa mama yake kwa miezi pungufu na bado akazaliwa vyema na kukua vyema.
Huko kote ni kukosea. Yesu alitungwa mimba na kukaa tumboni kama watoto wa kawaida wa wanadamu. Kwa kuwa tarehe ya 25 Desemba ni mapato ya utekaji sikukuu ya kipagani, kwa akili, ndio utamadunisho (rej. Mt 22:37), kusudi siku ya Mungu-jua wa wapagani itumike kumtukuzia Mungu Jua wa kweli yaani Yesu Kristo (rej. Yn 1:5-9), kutungwa kwake huadhimishwa kimahesabu nyuma, tarehe 25 Machi, ndiyo sikukuu ya Kupashwa Habari Bikira Maria. Tangu tarehe 25 Machi hadi 25 Desemba ni miezi tisa kamili. Hii ndiyo mantiki ya utamadunisho wa Kikristo.

Je, Kutamadunisha Kitu ni Halali?

Ni halali kabisa. Wapo wanaokasirika na kufoka kwa nini Wakristo walichukua tarehe ya wapagani, 25 Desemba kusherekea jambo la Kikristo. Watu kama hao ni wasahaulifu tu, usiwajali. Utamadunisho ni uchukuaji wa kitu fulani, kukipa maana mpya au nzuri zaidi na kukitumia. Wakristo hawawezi kukataa mambo ya wapagani wala wapagani hawawezi kukataa mambo ya Wakristo. Dunia ni moja, tunashirikishana. Wakristo hawana uwezo wa kuvumbua kila kitu chao. Tena hawapo Wakristo wa kanisa lolote waliovumbua vyote wanavyovitumia wenyewe. Asikudanganye mtu.
Kumbe, wanachogundua upande mmoja wa dunia, wewe wa upande mwingine unaweza kukichukua na kukitumia kwa manufaa yako. Cha wapagani kinaweza kutamadunishwa na Wakristo wakakitumia, na cha Wakristo kinaweza kuchukuliwa na Wapagani wakakitumia. Usinibishe.
Yafuatayo ni mambo ya uvumbuzi wa wapagani nasi tunatumia tena kwa furaha kabisa. Labda hatujui. Suruali, viatu, miwani, kioo, herufi, hesabu, kusoma na kuandika, matibabu ya hospitali n.k. Kama wewe ni mmoja wa wale wasiotaka kabisa mambo ya wapagani, usivitumie vitu hivi kuanzia kesho.

Huenda majibu haya yamekuzidi urefu. Lakini yasome moja moja kwa umakini mkubwa kama unataka kuujua ukweli. Kuyasoma majibu haya kwa umakini ndiyo gharama ya kujua tarehe ya kuzaliwa Bwana Yesu.
NAWATAKIENI NYOTE MAANDALIZI MEMA YA SIKUKUU YA KRISMASI. KILA LA HERI NYOTE!Fwatilia Website hii kupokea Makala Kama hii ya Sherehe na tarehe ya Kuzaliwa kwa Yesu Kristo

Endelea kusoma makala hizi za kufanana na hii ya; Sherehe na tarehe ya Kuzaliwa kwa Yesu Kristo

a.gif Mafundisho Kuhusu Bikira Maria

Kuna mafundisho makuu manne
kumhusu Bikira Maria ambayo ni lazima
kila Mkatoliki ayasadiki kutokana na
ufunuo wa Mungu: 1. B. Maria
mkingiwa dhambi ya asili 2. B. Maria
Mama wa Mungu 3. B. Maria Bikira
daima 4. B. Maria kupalizwa mbinguni
mwili na roho.. soma zaidi

a.gif Ukweli kuhusu tofauti na usawa wa X-MASS na CHRISTMAS

Na Fr. Titus Amigu
Lakini kwa leo nina jambo moja la kuweka sawa. Vijana kadhaa wameniomba nitoe maelezo kuhusiana na maneno “CHRISTMAS” na “X-MAS” maana wanachanganywa na wenzao. Kifupi, maelezo yanayosambazwa kwenye mitandao yetu ni kwamba “Christmas” ni sahihi na “X-mas” siyo sahihi. Maelezo haya yanayosambazwa si sahihi, ni ya uongo… soma zaidi

a.gif Weka Imani katika ahadi za Mungu

Utakavyo fanya kazi kwa bidii ndivyo utakavyo pata upenyo.Weka IMANI yako katika ahadi za MUNGU.. Badilisha mawazo yako katika kila utakacho kifanya na utafanikiwa hata kama umefanya Mara nyingi bila mafanikio…. soma zaidi

[Wimbo Mzuri PA.gif] Bwana ni nuru yangu

[Tafakari ya Sasa] 👉Njia ya Kumrudia Mungu

[Mtakatifu wa Sasa] 👉Mtakatifu Antoni wa Padua

[Jarida La Bure] 👉Sala za Asubuhi na Sala za Jioni

mtu-akifa-nini-hutokea.JPG

a.gif Dini ni nini?

Dini ndio mambo yatupasayo kwa Mungu Bwana wetu na Baba yetu. (Mk 16:15-16).. soma zaidi

a.gif Ni nani ameanzisha Kanisa Katoliki?

Yesu Kristo ameanzisha Kanisa Katoliki.. soma zaidi

a.gif Uzinzi na Uasherati ndio mtego wa kizazi hiki

Uzinzi na uasherati wakati huu umekuwa ndio sumaku kuu ya kuwanasa watu ili waende jehanamu… soma zaidi

a.gif Mambo makubwa yanayosababisha ndoa nyingi kuvunjika

Zifuatazo ni sababu kubwa za msingi zinzozifanya ndoa nyingi za kizazi cha Leo kuvunjika haraka na kukosa kudumu.. soma zaidi

a.gif Kutafuta dhambi maana yake ni nini?

Kutafuta dhambi maana yake ni kujiuliza moyoni dhambi nilizotenda Tangu ungamo la mwisho (Ef 4:17-32).. soma zaidi

a.gif Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zipi?

Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zote, kwa sababu upendo mtiifu wa Mwanae aliyejitoa kuwa sadaka ya wokovu wetu unampendeza kuliko dhambi zote zinavyomchukiza. Ila hatuwezi kusamehewa dhambi ya kukataa neema ambayo Roho Mtakatifu anatusukuma tuamini na kutubu, kwa sababu pasipo imani na toba hapana msamaha… soma zaidi

a.gif Usidanganyike Binti yangu

Binti mmoja alitaka ushauri kutoka kwa Mwalimu na maongezi yao yalikuwa hivi.. :
🔹 Binti : Shallom mwalimu..
🔹 Mwl : Shallom maranatha, binti yangu.
🔹 Binti : Mwl, kuna swali naomba nikuulize, maana linanisumbua sana kichwa changu.
🔹 Mwl : usijal binti yangu, karibu.
🔹 Binti : Mwl, mimi ni binti niliyeokoka na nampenda YESU, nina mchumba wangu ninampenda sana na yeye ananipenda pia, lakini yeye hajaokoka. Sasa ninaweza kuwa nae? Tuna malengo ya kuoana… soma zaidi

a.gif Elimu ni nini?

Ni maarifa ya kutambua werevu na udanganyifu wa shetani; anaposhawishi mwenyewe au kwa kutumia vitu au watu. (1Pet 5:8-9).. soma zaidi

a.gif Sakramenti ya Ekaristi Takatifu hukaa Tabernakulo kwa sababu gani

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu hukaa Tabernakulo kwa ajili ya watu wote hasa wagonjwa.. soma zaidi

a.gif Je, hatuwezi kupunguza mateso ya roho za marehemu waliokwenda toharani?

Ndiyo: twaweza kupunguza hata kuyamaliza kwa kuwasalia na kuwapatia rehema na hasa kwa kuadhimisha Misa kwa ajili yao. (2Mik 12:38-46).. soma zaidi

Fwatilia Website hii kwenye Email yako. Ingiza Email yako hapa kisha Bofya SUBSCRIBE na ufuate maelekezo

.

.

.

Website na, Melkisedeck Leon Shine | Tembelea website nyingine Hapa>>.