Sababu za gharika, Gharika na Agano la Mungu Na Noa

By, Melkisedeck Shine.

USIKOSE HII👉 Je, Biblia zote ni sawa?


Sababu za gharika, Gharika na Agano la Mungu Na Noa

Sababu za gharika

Mwanzo 6

1 Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao,

2 wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.

3 Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.

4 Nao Wanefili?b

5 Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.

6 Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.

7 Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya.

8 Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana.

9 Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu. Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu.

10 Nuhu akazaa wana watatu wa kiume, Shemu, na Hamu, na Yafethi.

11 Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma.

12 Mungu akaiona dunia, na tazama, imeharibika; maana kila mwenye mwili amejiharibia njia yake duniani.

13 Mungu akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia.

14 Ujifanyie safina ya mti wa mvinje; fanya na vyumba ndani ya safina, ukaifunike ndani na nje kwa lami.

15 Hivi ndivyo utakavyoifanya; mikono mia tatu urefu wa safina, mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini kwenda juu kwake.

16 Uifanyie safina mwangaza, ukaumalize juu kiasi cha mkono mmoja; ukautie mlango wa safina katika ubavu wake; ukaifanyie dari tatu, ya chini, ya pili, na ya tatu.

17 Na tazama, nitaleta gharika ya maji juu ya nchi, niharibu kila kitu chenye mwili na pumzi ya uhai, kisiwepo chini ya mbingu; kila kilichoko duniani kitakufa.

18 Lakini nitafanya agano langu nawe kuwa thabiti; nawe utaingia katika safina, wewe, na wanao, na mkeo, na wake za wanao, pamoja nawe.

19 Na katika kila kilicho hai chenye mwili, wawili wa kila namna utawaleta ndani ya safina, kuwahifadhi pamoja nawe; wawe mume na mke.

20 Katika vyote virukavyo kwa jinsi yake, na kila namna ya mnyama kwa jinsi yake, kila kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake, wawili wa kila namna watakuja kwako ili uwahifadhi.

21 Ukajitwalie chakula cha kila namna kinacholika, ukakusanye, nacho kitakuwa ni chakula chenu na chao.

22 Ndivyo alivyofanya Nuhu, sawasawa na vyote alivyomwamuru Mungu, hivyo ndivyo alivyofanya.

Gharika

Mwanzo 7

1 Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki.

2 Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke.

3 Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote.

4 Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arobaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali.

5 Nuhu akafanya kama vile Bwana alivyomwamuru.

6 Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi.

7 Nuhu akaingia katika safina, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kwa sababu ya maji ya gharika.

8 Na katika wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi,

9 wakaingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, mume na mke, kama vile Mungu alivyomwamuru Nuhu.

10 Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi.

11 Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka.

12 Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arobaini mchana na usiku.

13 Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye;

14 wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yo yote.

15 Waliingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake.

16 Na walioingia, waliingia mume na mke, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; Bwana akamfungia.

17 Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arobaini; nayo maji yakazidi, yakaieleza safina, ikaelea juu ya nchi.

18 Maji yakapata nguvu, yakazidi sana juu ya nchi; na ile safina ikaelea juu ya uso wa maji.

19 Maji yakapata nguvu sana sana juu ya nchi; na milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikizwa.

20 Maji yakapata nguvu, hata ikafunikwa milima kiasi cha mikono kumi na mitano.

21 Wakafa wote wenye mwili waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu;

22 kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu.

23 Kila kilicho hai juu ya uso wa nchi kikafutiliwa mbali tangu mwanadamu hata mnyama wa kufugwa, na kitambaacho, na ndege wa angani; vilifutiliwa mbali katika nchi, akabaki Nuhu tu, na hao walio pamoja naye katika safina.

24 Maji yakapata nguvu juu ya nchi siku mia na hamsini.

Mwisho wa Gharika

Mwanzo 8

1 Na Mungu akamkumbuka Nuhu, na kila kilicho hai, na wanyama wote waliokuwamo pamoja naye katika safina; Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakapungua;

2 chemchemi za vilindi zikafungwa, pia na madirisha ya mbinguni, mvua kutoka mbinguni ikazuiliwa;

3 maji yakadumu kuondoka katika nchi; na mwisho wa siku mia na hamsini maji yakapunguka.

4 Mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, safina ikatua juu ya milima ya Ararati.

5 Maji yakapunguka-punguka hata mwezi wa kumi; mwezi huo wa kumi, siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana.

6 Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya;

7 akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi.

8 Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi;

9 bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani.

10 Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili,

11 njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi.

12 Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe.

13 Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka.

14 Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu.

15 Mungu akamwambia Nuhu, akisema,

16 Toka katika safina, wewe, na mkeo, na wanao, na wake za wanao pamoja nawe.

17 Utoe pamoja nawe kila kilicho hai kilichomo pamoja nawe, chenye mwili, ndege, na mnyama, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi; wajae katika nchi, wawe na uzazi, wakaongezeke katika nchi.

18 Basi Nuhu akatoka, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye;

19 kila mnyama, na kila kitambaacho, na kila ndege, kila kinachokwenda juu ya nchi kwa kabila zao, wakatoka katika safina.

20 Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.

21 Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya.

22 Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.

Agano La Mungu na Noa

Mwanzo 9

1 Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi.

2 Kila mnyama wa katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu, na kila ndege wa angani: pamoja na vitu vyote vilivyojaa katika ardhi, na samaki wote wa baharini; vimetiwa mikononi mwenu.

3 Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu, kama nilivyowapa mboga za majani, kadhalika nawapeni hivi vyote.

4 Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile.

5 Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu.

6 Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.

7 Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni sana katika nchi, mkaongezeke ndani yake.

8 Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema,

9 Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu;

10 tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi.

11 Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi.

12 Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele;

13 Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi.

14 Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni,

15 nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili.

16 Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi.

17 Mungu akamwambia Nuhu, Hii ndiyo ishara ya agano nililoliweka kati yangu na wote wenye mwili walioko katika nchi.Fwatilia Website hii kupokea Makala Kama hii ya Sababu za gharika, Gharika na Agano la Mungu Na Noa

Endelea kusoma makala hizi za kufanana na hii ya; Sababu za gharika, Gharika na Agano la Mungu Na Noa

a.gif Waliozaliwa kutoka Adamu hadi Noa

1 Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya;.. soma zaidi

a.gif Kaini na Abeli

1 Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana… soma zaidi

a.gif Adamu na Eva Walivyotenda dhambi

1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia Eva, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?.. soma zaidi

[Wimbo Mzuri PA.gif] Haleluya

[Tafakari ya Sasa] 👉Tusali daima

[Mtakatifu wa Sasa] 👉Mtakatifu Justin mfiadini

a.gif Ishara za mafumbo zimetokana na nini?

Ishara za mafumbo zimetokana na viumbe (maji, mafuta, mkate, divai n.k.) na maisha ya jamii (kuosha, kupaka, kula na kunywa pamoja n.k.) na historia ya wokovu (kunyunyiza na kuzamisha, kuwekea mikono, kula Pasaka, n.k.),.. soma zaidi

a.gif Jina Yesu lina maana gani?

Jina Yesu lina maana kuwa "Mungu Anaokoa". (Mdo 4:12).. soma zaidi

a.gif Katika Amri ya Kwanza ya kanisa tumekatazwa nini?

Tumekatazwa;
1. Kukosa Misa
2. Kufanya kazi nzito siku hizo.. soma zaidi

a.gif Ijue Ishara ya Msalaba

Ishara ya Msalaba ni tendo la mtu kugusa paji la uso, kifua na mabega kwa kutumia mkono wa kulia na kutamka 'Kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina'… soma zaidi

a.gif Je, Mungu amewasiliana nasi?

Ndiyo, Mungu amewasiliana nasi, akijitambulisha na kujitoa kwetu, tuweze kuishi katika urafiki naye na hatimaye tushiriki heri yake… soma zaidi

a.gif Kujitambua Mbele ya Mungu

Kujitambua wewe ni nani na unanafasi gani mbele ya Mungu, hii ndio njia ya kuelekea Wokovu na Utakatifu… soma zaidi

a.gif Maneno na ishara kwenye ibada vinaweza kubadilishwa na nani?

Maneno na ishara vinaweza kubadilishwa na waandamizi wa Mitume, waliokabidhiwa na Yesu mamlaka ya kuendeleza kazi yake katika mazingira mbalimbali hata mwisho wa dunia… soma zaidi

a.gif Ufufuko wa wafu maana yake nini?

Ufufuko wa wafu maana yake mwisho wa dunia watu wote watafufuka na miili yao na kwenda nayo katika furaha ya milele au moto wa milele. (Ayu 19:25-26, Mt 22:30-32, Yh 28-29).. soma zaidi

a.gif Je, Kanisa linaweza kutuondolea dhambi yoyote?

Ndiyo, Kanisa linaweza kutuondolea dhambi yoyote katika ubatizo na kitubio kwa kutumia mamlaka ambayo Yesu mfufuka aliwashirikisha Mitume wake alipowavuvia akisema:.. soma zaidi

a.gif Malaika na watu wanaweza kuchagua hata nini?

Malaika na watu wanaweza kuchagua hata wawe wema au wabaya milele… soma zaidi

Fwatilia Website hii kwenye Email yako. Ingiza Email yako hapa kisha Bofya SUBSCRIBE na ufuate maelekezo

.

.

.

Website na, Melkisedeck Leon Shine | Tembelea website nyingine Hapa>>.